VIJANA WAHIMIZWA KUJIUNGA NA VIKUNDI ILI KUNUFAIKA NA FURSA ZA KIUCHUMI NA KUPAMBANA NA UMASKINI.
By Dayo Radio
Published on 20/06/2026 17:45 • Updated 20/06/2026 18:11
News

Vijana pamoja na wakazi wa kaunti ya Mombasa wamehimizwa kujiunga katika vikundi mbalimbali ili waweze kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotolewa na serikali pamoja na mashirika tofauti, hatua ambayo imetajwa kuwa muhimu katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira na kuimarisha maisha ya wananchi.

Wito huo umetolewa wakati wa shughuli ya kusafisha taka katika ufuo wa bahari ya Wangwani uliopo eneo la Junda, katika eneobunge la Kisauni, ambapo viongozi wa mashirika mbalimbali wamesisitiza umuhimu wa vijana kujipanga katika makundi ili kuwawezesha kupata mafunzo, mikopo pamoja na kushiriki katika miradi inayolenga kuinua hali zao za kiuchumi.

Akizungumza katika hafla hiyo, mwenyekiti na mwanzilishi wa shirika la JUNDA KASARANI REFORM (JKR), Victor Opondo, amesema kuwa kutokana na nafasi za ajira rasmi kuendelea kuwa chache, ni muhimu kwa vijana kuacha kutegemea ajira za kuajiriwa pekee na badala yake kuungana katika vikundi vinavyoweza kuwasaidia kubuni nafasi za kujiajiri.

Hata hivyo Opondo amesema kuwa kupitia vikundi hivyo, vijana wanaweza kupata ujuzi, kujengewa uwezo na kunufaika na programu mbalimbali zinazofadhiliwa na serikali na mashirika ya maendeleo, jambo ambalo litasaidia kupunguza kiwango cha umaskini katika jamii.

Aidha, amesema kuwa shirika la JKR limekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha uhifadhi wa mazingira kupitia mradi wa ukusanyaji na urejelezaji wa taka unaoendeshwa chini ya kauli mbiu ya "TAKA MALI", akibainisha kuwa taka zinaweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato iwapo zitatumika ipasavyo.

"Kwa sasa nafasi za ajira ni adimu, hivyo ni muhimu kwa vijana kujiunga katika vikundi ili waweze kunufaika na miradi mbalimbali inayotolewa na serikali na mashirika tofauti. Kupitia kauli mbiu yetu ya TAKA MALI, tunawahamasisha wananchi kuona taka kama rasilimali inayoweza kuleta kipato na kuboresha maisha yao," amesema Opondo.

Ameongeza kuwa suala la utunzaji wa mazingira halipaswi kuachwa mikononi mwa serikali pekee bali ni jukumu la kila mwananchi, akisema kuwa mazingira safi yanachangia afya bora na pia yanaweza kuwa chanzo cha ajira kwa maelfu ya vijana kupitia shughuli za ukusanyaji, upangaji na urejelezaji wa taka.

 

Kwa upande wake, meneja wa shirika la HAND IN HAND EASTERNAFRICA, Gerald Gichuki, amepongeza juhudi zinazofanywa na JKR katika kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira pamoja na kuwawezesha vijana kujipatia kipato.

 

Gichuki amesema kuwa shirika la HAND IN HAND EASTERN AFRICA linaamini kuwa uwezeshaji wa wananchi kupitia vikundi na miradi ya ubunifu ni njia mojawapo ya kupunguza umaskini na kuleta maendeleo endelevu katika jamii.

 

"Tunapongeza hatua iliyochukuliwa na shurika la JKR kwa kuwaleta pamoja wakazi na kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira huku wakijitengenezea kipato. Kama shirika la HAND IN HAND EASTERNAFRICA, tupo tayari kushirikiana na mashirika mengine yenye malengo yanayofanana ili kuhakikisha jamii zinapata fursa za kujikwamua kiuchumi kupitia ubunifu wa nafasi za ajira," amesema Gichuki.

 

Amesema ushirikiano kati ya mashirika ya kijamii, sekta binafsi na serikali ni muhimu katika kuhakikisha vijana wanapata fursa za mafunzo, mitaji na masoko ya bidhaa na huduma zao, hali ambayo itasaidia kujenga jamii yenye uwezo wa kujitegemea kiuchumi.

 

Wakati huohuo, wakazi wa eneo hilo wamehimizwa kuendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo na uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha jamii inanufaika na fursa mbalimbali zinazojitokeza.

 

Akizungumza kwa niaba ya wakazi, Nasoro Ngao amesema kuwa ushirikiano kati ya wananchi na mashirika mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha jamii inapata manufaa kutokana na miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi huku akitaja milango yake ipo wazi kwa yeyote anahitaji ushirikiano.

 

"Tunatoa wito kwa wakazi wote kujitokeza na kushiriki katika shughuli za maendeleo na uhifadhi wa mazingira. Kupitia umoja na ushirikiano, tunaweza kujenga jamii yenye mazingira safi na yenye uwezo wa kujitegemea kiuchumi," amesema Ngao.

 

Amesema kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha mazingira yanatunzwa na kuhimiza vijana kuchangamkia fursa zinazojitokeza kupitia vikundi vya kijamii na miradi mbalimbali ya maendeleo, akibainisha kuwa hatua hiyo itachangia katika kubuni nafasi zaidi za ajira na kuinua maisha ya wananchi.

 

Shughuli hiyo ya usafi wa mazingira katika ufuo wa Wangwani imewaleta pamoja wanajamii, vijana na wadau mbalimbali ambao wameshiriki katika ukusanyaji wa taka huku wakipewa elimu kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kutumia taka kama mali inayoweza kuleta manufaa ya kiuchumi. Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo wameeleza matumaini yao kuwa kupitia ushirikiano wa wadau tofauti, jamii itaendelea kunufaika na miradi ya maendeleo na hivyo kuchangia katika kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya wakaazi.

 

Na Harrison Kazungu.

Comments
Comment sent successfully!

Chat Online