TAKA NI MALI, VICTOR OPONDO AHIMIZA JAMII KUTUMIA TAKA KAMA FURSA YA KIUCHUMI.
By Dayo Radio
Published on 19/06/2026 10:35
News

Mwenyekiti na mwanzilishi wa shirika la kupambana na changamoto za mazingira la JUNDA KASARANI REFORM, Victor Opondo, amesema kuwa taka zina nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ikiwa zitatazamwa kama rasilimali badala ya kuwa mzigo kwa jamii.

Akizungumza wakati wa zoezi la kuwapa mafunzo vikundi mbalimbali kuhusu mbinu bora za usimamizi wa taka na namna ya kujinufaisha nazo, Ondero amesema kuwa shirika hilo kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali ikiwemo limekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu nasaha kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kutumia taka kubuni nafasi za ajira zitakazosaidia vijana kujikimu kimaisha.

Mafunzo hayo yameandaliwa chini ya kauli mbiu ya "TAKA MALI", ambayo inalenga kubadilisha mtazamo wa wakaazi wa Junda kuhusu taka na kuwahamasisha kuziona kama fursa ya kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali za urejelezaji na utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na taka.

Hata hivyo mwnye kiti huyo amesema kuwa miongoni mwa manufaa yanayoweza kupatikana kupitia usimamizi bora wa taka ni pamoja na kutengeneza ajira kwa vijana na wanawake, kujiongezea kipato kupitia biashara ya taka zinazoweza kurejelewa, kupunguza uchafuzi wa mazingira pamoja na kusaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

"Taka zina thamani kubwa iwapo zitashughulikiwa kwa njia inayofaa. Badala ya kuzitupa kiholela na kusababisha uchafuzi wa mazingira, wananchi wanapaswa kuzitumia kama fursa ya kujipatia kipato na kuboresha maisha yao. Hii ndiyo maana ya kauli mbiu yetu ya 'TAKA MALI'," amesema Opondo.

Aidha, amesema zoezi hili linaendelea kwa wiki moja na elimu hiyo inalenga kuijengea jamii uwezo wa kutambua nafasi yake katika kuhifadhi mazingira na kuhakikisha kuwa maeneo wanayoishi yanakuwa safi na salama kwa afya ya wananchi.

Katika mafunzo hayo, Opondo ametoa shukrani kwa Serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa ushirikiano ambao imekuwa ikitoa katika kufanikisha shughuli mbalimbali za mazingira, akisema kuwa msaada huo umekuwa chachu ya kufanikisha juhudi za kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa usafi na uhifadhi wa mazingira.

"Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa kuendelea kushirikiana nasi katika juhudi hizi muhimu.Ushirikiano huu umewezesha kufikisha elimu kwa wananchi wengi zaidi na kuimarisha shughuli za uhifadhi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya kaunti hii," amesema.

Vilevile, ametoa wito kwa wananchi kuachana na tabia ya kutupa taka kiholela, akisisitiza kuwa tabia hiyo imekuwa ikichangia kuziba kwa mifereji ya maji, kuenea kwa magonjwa pamoja na kuharibu mazingira.

"Ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anazingatia usafi wa mazingira kwa kutupa taka katika maeneo yaliyotengwa na kushiriki katika shughuli za urejelezaji. Tukifanya hivyo tutakuwa tunajenga jamii yenye afya bora na mazingira salama," ameongeza.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Florence Ngao, ambaye ni mmoja wa mabalozi wa mitaa, aliyesisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha mji wa Mombasa unabaki kuwa safi.

Florence amesema kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na mashirika ya kijamii na serikali, bado kuna haja ya wahisani na washirika wa maendeleo kuingilia kati kwa kutoa vifaa na rasilimali zinazohitajika ili kuendeleza kampeni za usafi wa mazingira.

"Tunatoa wito kwa wahisani na wadau mbalimbali kujitokeza na kuunga mkono juhudi hizi kwa kutoa vifaa vinavyohitajika ili kuwezesha shughuli za ukusanyaji na usimamizi wa taka. Ushirikiano wa kila mmoja ni muhimu katika kuhakikisha tunadumisha usafi wa mji wa Mombasa," amesema Florence Ngao.

Aidha, amewahimiza wakazi wa Mombasa kuwa mstari wa mbele katika kutunza mazingira yao na kushiriki kikamilifu katika mipango mbalimbali inayolenga kuboresha usafi wa maeneo wanayoishi.

Mafunzo hayo yamewakutanisha wanachama wa vikundi mbalimbali vya kijamii pamoja na wadau wa mazingira, huku yakilenga kuhamasisha matumizi bora ya taka kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii, sambamba na kuendeleza juhudi za kuifanya Kaunti ya Mombasa kuwa safi na yenye mazingira bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!

Chat Online