SENETA WA NAIROBI EDWIN SIFUNA AONDOLEWA KATIKA KAMATI YA NISHATI YA SENETI, ASISITIZA KUENDELEA KUTETEA MASLAHI YA WANANCHI.
By Dayo Radio
Published on 18/06/2026 07:07
News

Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, ameondolewa katika kamati ya Nishati ya Seneti inayoongozwa na Seneta Oburu Oginga, hatua ambayo imezua mjadala mkali wa kisiasa ndani ya Chama cha ODM.

Akizungumza baada ya kuondolewa kwake, Sifuna amesema kuwa ataendelea kutekeleza majukumu yake kama Seneta wa Nairobi na kuwatetea wananchi bila kuyumbishwa na mabadiliko ya kamati za Bunge.

"Nitaendelea kutekeleza majukumu yangu kama Seneta wa Nairobi na kutetea maslahi ya wananchi bila kuyumbishwa na mabadiliko ya kamati za Bunge," amesema Sifuna.

Aidha, Sifuna amesisitiza umuhimu wa kuheshimu viongozi wenye misimamo tofauti kuhusu masuala ya kitaifa, akibainisha kuwa tofauti za maoni hazipaswi kuwa sababu ya kuadhibiwa au kutengwa kwa viongozi wanaotekeleza majukumu yao ya umma.

"Viongozi wanapaswa kuheshimiwa kwa misimamo yao tofauti katika masuala ya kitaifa," ameongeza.

Hatua hiyo imekuja miezi kadhaa baada ya Sifuna kuondolewa katika nafasi ya katibu mkuu wa ODM, huku akihusishwa mara kwa mara na kauli zilizokosoa baadhi ya maamuzi ya chama hicho.

Kuondolewa kwake katika kamati ya Nishati ya Seneti kumeibua hisia tofauti miongoni mwa viongozi na wafuasi wa kisiasa, ambapo baadhi wanaona kuwa ni sehemu ya mabadiliko ya kawaida ya kamati za Bunge, huku wengine wakitafsiri hatua hiyo kuwa huenda inahusiana na misimamo yake kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa.

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!

Chat Online