Zaidi ya wanafunzi 400 walihitimu katika mahafali ya 10 ya chuo cha kiufundi cha Kisauni (Kisauni Vocational Training Centre)huku viongozi wa taasisi hiyo wakisisitiza umuhimu wa elimu ya ufundi katika kuwawezesha vijana kujitegemea na kujiepusha na uhalifu.

Akizungumza katika hafla hiyo Mwalimu Mkuu wa chuo hicho Hadija Abdallah, alisema ana furaha kubwa kuona zaidi ya wanafunzi 400 wakihitimu baada ya kukamilisha mafunzo yao katika fani mbalimbali za ufundi.
“Nina furaha adhimu kuona wanafunzi wetu wakihitimu leo. Hii ni ishara kuwa juhudi zao na za walimu zimezaa matunda"

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo Athman Omar Chai, alisema licha ya changamoto mbalimbali zilizokumba taasisi hiyo katika safari yake ya kutoa mafunzo, ni jambo la kujivunia kuona mahafali hayo yakifanyika kwa mafanikio.

"Licha ya changamoto nyingi lakin mwishowe tumeweza kufanikiwa kuwezesha tamasha hili , ninafuraha sana na nawaombea vijana hawa wapate mazuri baada ya kuhitimu"
Mgeni wa heshima katika hafla hiyo Nelson Alfayo ambaye ni mmoja wa wanaowania ubunge katika eneobunge la Nyali, aliwahimiza vijana kuthamini elimu na kutumia ujuzi wanaoupata kujijengea maisha bora ili waweze ili kujiepusha na vitendo vya uhalifu na matumizi ya mihadarati, ambayo alisema yanaendelea kuathiri vijana wengi nchini.

“Vijana wanapaswa kushikilia elimu na kutumia ujuzi wao kujiletea maendeleo na wajinasue kwenye mitaro ambayo inaangamiza vijana katika jamii"
Wakati uo huo mmoja wa wazazi waliohudhuria hafla hiyo aliwahimiza wazazi wengine kuwapeleka watoto wao katika vyuo vya ufundi ili wapate stadi zitakazowasaidia kujitegemea.
" kwa wale wazazi ambao hawajawapeleka watoto wao katika vyuo vya ufundi ningewahimiza wajitahidi kuwapeleka watoto katoka vyuo vya ufundi "
Nao baadhi ya wahitimu wa chuo hicho waliwataka vijana wenzao kujiunga na taasisi za mafunzo ya ufundi, wakisema elimu ya ufundi huwapa maarifa ya kujiajiri, kujikimu kimaisha na kujiepusha na ushawishi wa magenge ya uhalifu.

"Ningependa kuwaambia vijana wenzangu kwamba vyuo vya ufundi vinasaidia sana na wawe na subra sana katika hakuna ujuzi unaoenda mkono mtupu"

Mahafali hayo yaliangazia mchango mkubwa wa elimu ya ufundi katika kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kuchangia maendeleo ya jamii