Taasisi ya Masoroveya humu nchini(ISK) imeeleza wasiwasi wake kuhusu hatua ya ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (ODPP) kuwafungulia mashtaka wanachama wa kamati ya kiufundi ya mipango miji ya kaunti ya Nairobi (UPTC) kuhusiana na kuporomoka kwa jengo la Manzil Towers, ikisema kuwa uwajibikaji unapaswa kuzingatia ushahidi na wajibu wa kila mtu binafsi badala ya kuwahusisha wote kwa pamoja. Katika taarifa kwa vyombo vya habari ,ISK imetoa rambirambi zake kwa familia za waathiriwa wa mkasa huo na kusisitiza kuwa inaunga mkono hatua za kuhakikisha wale waliohusika na vitendo vya uzembe, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka au ukiukaji wa maadili ya kitaaluma wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
"Uwajibikaji lazima uzingatie sheria, ushahidi, wajibu wa taasisi na hatia ya mtu binafsi. Haupaswi kutekelezwa kupitia kuwahusisha watu wote kwa pamoja au kwa hatua zinazoficha matatizo ya kimfumo yanayoendelea kuathiri mchakato wa mipango na udhibiti wa maendeleo katika Kaunti ya Nairobi," imesema ISK.
Taasisi hiyo aidha imefafanua kuwa Kamati ya UPTC ina jukumu la kutoa ushauri wa kitaalamu pekee na haina mamlaka ya kuidhinisha maendeleo au kutekeleza hatua za kisheria.
"Kamati ya kiufundi ya mipango Miji (UPTC) ina jukumu la ushauri pekee. Haitoi vibali vya maendeleo, haitoi vyeti vya matumizi ya majengo na haina mamlaka ya utekelezaji," imeeleza taasisi hiyo.
Hata hivyo ISK imeonya kuwa kuwahusisha wanachama wote wa kamati hiyo katika mashtaka kunakiuka misingi ya haki na uwajibikaji wa mtu binafsi.
"Haki inahitaji uwajibikaji wa jinai kuzingatia mtu mmoja mmoja. Kila mtu anapaswa kuwajibishwa kwa matendo aliyoyafanya, kuidhinisha au kuficha, na si kwa sababu tu ya kuwa mwanachama wa jukwaa la ushauri," imesema ISK.
Aidha, imeonya kuwa hatua hiyo inaweza kuwakatisha tamaa wataalamu kushiriki katika mifumo ya usimamizi wa umma.
"Kuwafungulia mashtaka ya pamoja wawakilishi wa kitaalamu wanaoshiriki katika jukwaa la mapitio ya kiufundi kunaunda mfano hatari ambao unaweza kuwakatisha tamaa wataalamu wenye sifa kushiriki katika mifumo ya usimamizi na utawala wa umma," imeongeza.
Kuhusu hatua ya gavana wa Nairobi kuunda upya kamati ya UPTC, ISK imesema mabadiliko hayo pekee hayawezi kutatua changamoto zilizopo katika mfumo wa usimamizi wa maendeleo.
"Kubadilisha wajumbe wa kamati hakuwezi kuchukuliwa kuwa mageuzi ya kweli ya taasisi wala kuwa suluhisho la changamoto za muda mrefu katika utawala wa mipango miji," imesema taasisi hiyo.
Wakayi uo huo ISK imesema kuwa mkasa wa Manzil Towers umefichua udhaifu mkubwa katika mfumo wa usimamizi wa maendeleo na kusisitiza kuwa hatua za muda mfupi hazitazuia majanga kama hayo kutokea tena.
"Iwapo mapungufu ya kimfumo hayatashughulikiwa, kubadilisha kamati au kuwafungulia mashtaka baadhi ya watu hakutazuia majanga kama haya kutokea tena," imesema.
Taasisi hiyo pia imeitaka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuhakikisha kuwa hatua zozote za kisheria zinaongozwa na ushahidi wa moja kwa moja.
"Uwajibikaji wa jinai unapaswa kuwekwa pale ambapo ushahidi unaonyesha ushiriki wa moja kwa moja katika makosa. Haki inapaswa kulenga vitendo vya ukiukaji, si ushiriki katika chombo cha ushauri," imesisitiza ISK.
Taasisi hiyo imesema itaendelea kuunga mkono maendeleo yanayozingatia sheria, uadilifu wa kitaaluma, usalama wa umma na mageuzi yatakayosaidia kuimarisha taasisi zinazolinda maslahi ya wananchi.
NA HARRISON KAZUNGU.