Serikali ya Kenya imesisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama wa baharini kupitia ushirikiano wa kimataifa ili kukabiliana na vitisho mbalimbali vinavyoendelea kuathiri biashara ya kimataifa na usafiri wa majini.
Akifungua rasmi mkutano wa nne wa Kamati ya Uongozi ya Jukwaa la Kubadilishana Taarifa za Kanda ya Indo-Pacific (IORIS) uliofanyika jijini Mombasa, Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, Kipchumba Murkomen, amesema kuwa usalama wa bahari una mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa mataifa na kuhakikisha shughuli za biashara duniani zinaendelea bila vikwazo.
Murkomen amesema kuwa bahari salama ni nguzo muhimu ya ustawi wa kiuchumi, hasa ikizingatiwa kuwa sehemu kubwa ya biashara ya kimataifa hutegemea njia za usafiri wa majini. Ameongeza kuwa kulinda njia hizo ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa karibu kati ya mataifa na taasisi mbalimbali za kikanda na kimataifa.
Waziri huyo amesisitiza kuwa vitisho vya kiusalama vinavyoendelea kujitokeza katika maeneo ya bahari, ikiwemo uharamia baharini, uporaji wa meli, uvuvi haramu, usafirishaji haramu wa bidhaa pamoja na utupaji wa taka hatari baharini, vinaendelea kuhatarisha usalama wa mataifa na kuathiri mtiririko wa biashara na uchumi wa dunia.
Amesema changamoto hizo zimeongeza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kubadilishana taarifa za kiusalama na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa ili kuwezesha mataifa kukabiliana kwa pamoja na vitisho vinavyoibuka.
Murkomen pia amesisitiza haja ya matumizi ya teknolojia na mifumo ya kisasa ya ukusanyaji na ubadilishanaji wa taarifa ili kuongeza uwezo wa mataifa kufuatilia na kudhibiti shughuli haramu zinazofanyika katika maeneo ya bahari.
Wakati huo huo, Waziri huyo amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Kenya na Umoja wa Ulaya kupitia mradi wa Critical Maritime Routes Indo-Pacific (CRIMARIO), akisema kuwa mpango huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uwezo wa taasisi mbalimbali nchini katika kushughulikia changamoto za usalama wa baharini.
Amesema kupitia mradi huo, Kenya imefanikiwa kuimarisha uratibu kati ya taasisi zinazohusika na masuala ya baharini pamoja na kuongeza uwezo wa kubadilishana taarifa muhimu za kiusalama na washirika wa kimataifa.
Murkomen ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na mataifa mengine pamoja na wadau mbalimbali ili kuhakikisha njia za usafiri wa majini zinabaki salama, jambo ambalo litachochea ukuaji wa biashara, kulinda uchumi wa mataifa na kuimarisha maendeleo endelevu duniani.
Mkutano huo wa nne wa Kamati ya Uongozi ya Jukwaa la IORIS umezikutanisha nchi wanachama na wadau mbalimbali kujadili namna ya kuimarisha usalama wa baharini kupitia ushirikiano, ubadilishanaji wa taarifa na matumizi ya mifumo ya kisasa katika kukabiliana na vitisho vinavyoathiri sekta ya bahari katika eneo la Indo-Pacific na kwingineko duniani.
NA HARRISON KAZUNGU.