BUNGE LAKUSANYA MAONI YA WANANCHI KUHUSU MSWADA WA FEDHA 2026 MOMBASA
By Dayo Radio
Published on 08/06/2026 15:55
News

Kamati ya bunge la kitaifa kuhusu fedha na mipango ya kitaifa imeendelea na zoezi la ushirikishwaji wa umma kuhusu mswada wa fedha wa mwaka 2026, ambapo imekutana na wananchi wa kaunti ya Mombasa ili kukusanya maoni, mapendekezo na hoja mbalimbali zinazolenga kuboresha mswada huo kabla ya kujadiliwa na kupitishwa bungeni.

Kikao hicho kimeongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Molo, Kimani Kuria, ambaye amesema kuwa ushiriki wa wananchi katika mchakato wa kutunga sheria ni muhimu kwa kuwa unatoa nafasi kwa wakenya kutoa maoni yao kuhusu sera na hatua zinazoweza kuathiri maisha yao ya kila siku.

"Tumepokea maoni na mapendekezo mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu vipengele tofauti vya mswada wa fedha wa mwaka 2026. Baadhi ya mapendekezo hayo yanahitaji uchambuzi wa kina zaidi huku mengine yakitarajiwa kufanyiwa kazi mara moja. Kamati itazingatia maoni yote yaliyowasilishwa na kuyapeleka bungeni kwa mjadala zaidi."

Ameongeza kuwa dhamira ya kamati ni kuhakikisha kuwa sauti za wananchi zinasikika n kupewa uzito unaostahili katika mchakato wa kutunga sheria za kifedha ambazo zina athari kwa uchumi wa taifa na maisha ya wananchi.

Wananchi waliohudhuria kikao hicho wametoa maoni kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo ushuru, gharama ya maisha, mazingira ya biashara, uwekezaji, ajira kwa vijana na matumizi ya fedha za umma. Wengi wao wamesisitiza umuhimu wa serikali kuweka sera zitakazochochea ukuaji wa uchumi huku zikilinda maslahi ya wananchi wa kawaida.

Mbali na masuala ya Mswada wa Fedha wa mwaka 2026, Kuria pia alizungumzia changamoto zinazowakabili baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA) kuhusiana na malipo ya mafao yao ya uzeeni.

"Suala la pensheni za wafanyakazi wa KPA ni jambo muhimu ambalo linahitaji kushughulikiwa kwa umakini. Tutashirikiana na wadau wote husika ili kupata suluhu ya kudumu na kuhakikisha kuwa kila mfanyakazi anayestahili mafao yake anayapata kwa wakati na kwa mujibu wa sheria."

Kauli hiyo imepokelewa vyema na baadhi ya wafanyakazi na wastaafu wa KPA ambao kwa muda wamekuwa wakitaka kupatikana kwa suluhisho la changamoto zinazohusiana na mafao yao ya uzeeni.

Kikao hicho ni sehemu ya mchakato unaoendelea kote nchini wa kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Mswada wa Fedha wa mwaka 2026 kabla ya kuwasilishwa rasmi bungeni kwa mjadala na maamuzi ya mwisho. Kamati hiyo imesisitiza kuwa ushirikishwaji wa umma utaendelea kuwa sehemu muhimu ya kuhakikisha sheria zinazopitishwa zinazingatia mahitaji na matarajio ya wananchi.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!

Chat Online