VIONGOZI WA KIDINI WAPONGEZA HATUA YA RAIS RUTO YA KUTAMBUA ELIMU YA DUKSI NA MADRASSA KATIKA MFUMO RASMI WA ELIMU.
By Dayo Radio
Published on 02/06/2026 15:58
News

Viongozi wa kidini jijini Mombasa chini ya mwavuli wa Pwani Patriotic Religious Leaders (PPRL) wamepongeza kauli ya Rais William Ruto ya kutambua na kujumuisha elimu ya Duksi na Madrassa katika mfumo rasmi wa elimu nchini, wakisema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha maadili, mshikamano wa kijamii na kukuza usawa katika upatikanaji wa elimu.Wakizungumza na wanahabari jijini Mombasa, viongozi hao wakiongozwa na Sheikh Abu Qatada wameeleza kuwa elimu ya dini ina mchango mkubwa katika kumjenga mtoto kiimani, kimaadili na kijamii, sambamba na kumuwezesha kumjua Mwenyezi Mungu tangu akiwa mdogo.

Sheikh Abu Qatada amesema elimu ya Duksi na Madrassa imekuwa msingi muhimu wa malezi ya watoto katika jamii nyingi, kwani huwasaidia kujifunza misingi ya dini, kuheshimu wazazi na jamii, pamoja na kuzingatia maadili mema yanayochangia kujenga taifa lenye nidhamu.

“Elimu ya Duksi na Madrassa imekuwa na mchango mkubwa katika kuwajenga watoto kiimani na kimaadili. Uamuzi wa kuitambua na kuijumuisha katika mfumo rasmi wa elimu ni hatua muhimu itakayosaidia kukuza maadili mema na kuhakikisha watoto wote wanapata fursa sawa ya elimu nchini,” amesema Sheikh Abu Qatada.

Ameongeza kuwa, tofauti na mtazamo wa baadhi ya watu, elimu ya dini haipingani na elimu ya kawaida bali inaongeza msingi wa maadili unaosaidia mwanafunzi kuwa na mwenendo mzuri katika maisha ya kila siku.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Sheikh Hassan Mubarak, Mwenyekiti wa Muungano wa Maimamu na Walimu wa Madrassa katika kata ndogo ya Kilifi Kusini, ambaye amesema hatua hiyo ni ya kihistoria kwa jamii ya Kiislamu nchini na inalenga kuimarisha ujumuishi katika sekta ya elimu.

Sheikh Mubarak amesema kutambuliwa kwa elimu ya Duksi na Madrassa kutasaidia kupunguza changamoto za watoto wengi walioko katika mazingira magumu ya kiuchumi, ambao mara nyingi hukosa fursa sawa za elimu rasmi.

“Tunaiomba Wizara ya Elimu kuharakisha utekelezaji wa mwongozo huu ili wanafunzi wanaosoma katika Duksi na Madrassa wanufaike kikamilifu. Hatua hii itasaidia watoto wengi, hususan kutoka familia zenye changamoto za kiuchumi, kupata elimu bora na yenye usawa,” amesema Sheikh Hassan Mubarak.

Ameongeza kuwa utekelezaji mzuri wa sera hiyo utaimarisha mshikamano wa kitaifa, kupunguza pengo la elimu, na kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata nafasi ya kujifunza bila kubaguliwa kutokana na mfumo wa elimu anaoupitia.

Viongozi hao kwa pamoja wameeleza matumaini yao kuwa hatua hiyo ya serikali itaendelea kuchangia kujenga jamii yenye maadili bora, kuongeza ushirikiano wa kidini na kitaifa, na kuimarisha nafasi ya elimu ya dini katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Comments
Comment sent successfully!

Chat Online