VIONGOZI WA KIDINI MOMBASA WAMTETEA OMAR HASSAN SARAI DHIDI YA SHINIKIZO LA KUJIUZULU.
By Dayo Radio
Published on 29/05/2026 06:19
News

Viongozi wa kidini jijini Mombasa chini ya Pwani Patriotic Religious Leaders (PPRL) wamemtetea Katibu Mkuu wa Chama cha UDA Omar Hassan Sarai dhidi ya shinikizo la kumtaka ajiuzulu kufuatia matamshi yake ambayo yamezua mjadala wa kisiasa nchini.

Wakizungumza na wanahabari, viongozi hao wakiongozwa na Sheikh Abuu Qatada, wamewataka wanasiasa kuepuka unafiki wa kisiasa na badala yake kushughulikia changamoto za msingi zinazowakabili wananchi, hasa suala la ardhi ambalo wamesema ni tatizo la muda mrefu katika ukanda wa Pwani.

Sheikh Abuu Qatada amesema kuwa kauli ya Sarai haikupaswa kutafsiriwa kwa mtazamo wa mgawanyiko wa kikabila, bali ililenga kuibua mjadala kuhusu masuala yanayogusa maisha ya wananchi wa Pwani.

Aidha, mkereketwa Ali Hassan Tito amemtaka Katibu Mkuu huyo wa UDA kutojiuzulu, akisisitiza kuwa anapaswa kuendelea kutetea maslahi ya wakazi wa Pwani katika ngazi ya kitaifa. Amesema kuwa viongozi wanapaswa kupewa nafasi ya kueleza changamoto za jamii badala ya kushinikizwa kimyakimya.

Kauli za viongozi hao wa kidini zinajiri kufuatia baadhi ya viongozi wa Chama cha UDA kumpa jatibu mkuu huyo makataa ya saa 48 ajiuzulu, wakidai kuwa matamshi yake yalilenga kuibagua jamii ya Mlima Kenya. Viongozi hao sasa wanaitaka serikali na vyama vya siasa kushughulikia tofauti hizo kwa njia ya mazungumzo na maridhiano badala ya makabiliano ya kisiasa.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!

Chat Online