Waziri wa utalii na biashara kaunti ya Mombasa Mohamed Osman Ali amekanusha madai ya kamati inayosimamia wafanyibiashara na shughuli za soko la Kongowea kwamba serikali ya kaunti imekuwa ikiingilia majukumu ya viongozi wa soko hilo.
Akizungumza katika mahojiano ya kipekee, Waziri Osman amesema madai yanayoibuliwa kwa sasa hayana msingi wowote, akieleza kuwa wanachama wanaolalamika walihusika kikamilifu katika mchakato wa uteuzi wa kamati ya muda inayosimamia shughuli za soko hilo.
“Hakuna wakati wowote ambapo serikali ya kaunti imeingilia majukumu ya viongozi wa soko la Kongowea. Wale wanaotoa malalamishi walishiriki kikamilifu katika mchakato wa uteuzi wa kamati ya muda, hivyo ni jambo la kushangaza kuona madai kama hayo yakitolewa sasa,” amesema Osman.
Waziri huyo amesema serikali ya Kaunti ya Mombasa imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na wafanyibiashara wa soko la Kongowea kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wafanyibiashara pamoja na wananchi wanaotegemea soko hilo.
Aidha ametaja madai yanayotolewa na baadhi ya wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na katibu mratibu Elijah Kithela hayana mashiko na yanaweza kuathiri juhudi zinazoendelea za kuleta maendeleo katika soko hilo kubwa la biashara ndani ya Kaunti ya Mombasa.
“Serikali ya kaunti haina nia yoyote ya kuwachagulia wafanyibiashara viongozi wao. Kazi yetu ni kuhakikisha kuna mazingira bora ya biashara, usafi, usalama na huduma zinazowawezesha wafanyibiashara kufanya shughuli zao kwa utulivu,” ameongeza Waziri Osman.
Aidha, Waziri Osman amepuzilia mbali madai kwamba kuna mpango wa kufanya uchaguzi mpya mwaka wa 2028 ili kuchagua viongozi wapya wa soko hilo kupitia kura za wafanyibiashara.
Amesema taarifa hizo si rasmi na kwamba serikali ya kaunti haijatoa tangazo lolote kuhusu uchaguzi huo, akiwataka wafanyibiashara kupuuza taarifa zinazoweza kuzua taharuki au mgawanyiko ndani ya soko hilo.
“Tunawasihi wafanyibiashara wa kongowea kuendelea kuwa watulivu na kushirikiana na serikali ya kaunti. Hatutaki siasa wala migogoro ambayo inaweza kurudisha nyuma maendeleo yanayoendelea kushuhudiwa katika soko hili,” amesema.
Waziri huyo amesema serikali ya Kaunti ya Mombasa imewekeza fedha nyingi katika miradi ya kuboresha miundombinu ya soko la Kongowea, ikiwemo uboreshaji wa mifumo ya maji, usafi, maeneo ya biashara na usalama wa wafanyibiashara pamoja na wateja.
Hata hivyo ameeleza kuwa hatua hizo zinalenga kuinua hadhi ya soko la Kongowea ili liweze kuwa kitovu bora cha biashara katika ukanda wa Pwani na kuvutia wawekezaji zaidi pamoja na kuongeza mapato ya wafanyibiashara.
“Tumetenga fedha nyingi kuhakikisha soko la Kongowea linakuwa katika hali bora zaidi. Tunataka wafanyibiashara wanufaike kupitia mazingira mazuri ya biashara na huduma bora ambazo zitawasaidia kukuza shughuli zao za kiuchumi,” amesema Osman.
Waziri Osman amehitimisha kwa kuwataka wafanyibiashara wa soko hilo kushirikiana na serikali ya kaunti pamoja na viongozi waliopo ili kuhakikisha juhudi za maendeleo zinafanikiwa kwa manufaa ya kila mmoja anayelitegemea soko la Kongowea.
NA HARRISON KAZUNGU.