RUTO AKABIDHI HATI MILIKI MOMBASA KATIKA JUHUDI ZA KUTATUA MGOGORO WA ARDHI PWANI.
By Dayo Radio
Published on 21/05/2026 11:30
News

Rais William Ruto leo yuko katika Mombasa kwa hafla kubwa ya utoaji wa hati miliki za ardhi inayofanyika katika eneo la Mama Ngina Waterfront.

Hafla hiyo ni sehemu ya mpango wa serikali ya Kenya Kwanza wa kuharakisha utoaji wa hati miliki katika ukanda wa Pwani, eneo ambalo kwa muda mrefu limekumbwa na changamoto za umiliki wa ardhi, migogoro ya mashamba pamoja na visa vya unyakuzi wa ardhi.

Katika ziara hiyo, Rais Ruto anatarajiwa kukabidhi maelfu ya hati miliki kwa wakazi kutoka maeneo mbalimbali ya Pwani huku akisisitiza dhamira ya serikali kuhakikisha wananchi wanapata haki yao ya kumiliki ardhi kihalali.

Serikali imeeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto za kihistoria ambazo zimekuwa zikisababisha migogoro ya mara kwa mara kati ya wakazi na wawekezaji pamoja na kuzuia visa vya wananchi kunyanyaswa kutokana na ukosefu wa nyaraka rasmi za umiliki wa ardhi.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Waziri wa Madini Hassan Joho, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir, Waziri wa Michezo Salim Mvurya, Spika wa Seneti Amason Kingi pamoja na Naibu Rais Kithure Kindiki.

Viongozi hao wamepongeza juhudi za serikali katika kutatua changamoto ya ardhi katika ukanda wa Pwani wakisema kuwa umiliki rasmi wa ardhi utachangia kuimarisha maendeleo ya kiuchumi, kuongeza thamani ya mali za wananchi pamoja na kuvutia uwekezaji katika eneo hilo.

Aidha, serikali imesema kuwa imetenga zaidi ya shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya uchakataji wa hati miliki pamoja na ununuzi wa ardhi kutoka kwa wamiliki wasioishi nchini ili kuwasaidia wakazi wa Pwani kupata umiliki rasmi wa mashamba wanayoishi kwa miaka mingi.

Rais Ruto pia anatarajiwa kueleza hatua nyingine ambazo serikali inapanga kuchukua ili kuhakikisha migogoro ya ardhi katika maeneo ya Pwani inatatuliwa kabisa na wananchi wanapata usalama wa umiliki wa ardhi yao.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!

Chat Online