MAHAKAMA KUU YABATILISHA UTEUZI WA AISHA JUMWA KAMA MWENYEKITI WA BODI YA BARABARA ZA KITAIFA.
By Dayo Radio
Published on 20/05/2026 18:48
News

Pigo kubwa limempata aliyekuwa Waziri wa zamani Aisha Jumwa baada ya Mahakama Kuu kubatilisha rasmi uteuzi wake kama mwenyekiti wa bodi ya kitaifa ya barabara nchini.

 

Katika uamuzi uliotolewa na Jaji Bahati Mwamuye, mahakama imesema kuwa mchakato uliotumika kumteua Jumwa haukuzingatia matakwa ya sheria pamoja na misingi ya uwazi, ushindani wa haki na uwajibikaji katika ajira za umma kama inavyotakiwa na Katiba ya Kenya.

 

Jaji Mwamuye alieleza kuwa uteuzi wa viongozi wa taasisi za umma lazima ufanywe kwa njia iliyo wazi na inayowapa Wakenya wote nafasi sawa ya kuwania nyadhifa hizo, akiongeza kuwa serikali inapaswa kuzingatia kikamilifu taratibu za kisheria kabla ya kufanya uteuzi wowote wa umma.

 

Mahakama imefuta notisi mbili za serikali zilizokuwa zimemteua Jumwa kushikilia wadhifa huo, hatua inayomaanisha kuwa hatatambuliwa tena kisheria kama mwenyekiti wa bodi hiyo.

 

Hata hivyo, mahakama imebainisha kuwa maamuzi yote yaliyofanywa wakati akiwa afisini yataendelea kubaki halali ili kuhakikisha shughuli za taasisi hiyo haziathiriki na kulinda maslahi ya umma.

 

Aidha, mahakama imeagiza serikali kuanzisha upya mchakato wa uteuzi kwa kuufuata kikamilifu sheria, katiba pamoja na misingi ya haki na uwazi.

 

Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani na mwanaharakati Francis Owino ambaye alipinga uteuzi wa Jumwa akidai kuwa haukufuata utaratibu unaotakiwa katika uteuzi wa viongozi wa taasisi za umma.

 

Uamuzi huo sasa unatarajiwa kuzua mjadala mkubwa kuhusu namna serikali inavyofanya uteuzi wa viongozi katika mashirika na taasisi mbalimbali za umma nchini.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!

Chat Online