Taasisi ya Masoroveya nchini, ISK, imeitaka mamlaka ya elimu na ufundi (TVETA) pamoja na Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) kuangazia kwa makini ubora wa kozi za usoroveya zinazotolewa katika vyuo mbalimbali nchini ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mafunzo yanayokidhi viwango vya kitaaluma.
Akizungumza mjini Mombasa katikaka kongamano la siku tatu lililowakutanisha washikadau wa sekta ya usoroveya, rais wa taasisi hiyo Erick Nyadimo amesema kuna baadhi ya taasisi za elimu zinazoendelea kutoa mafunzo hayo kupitia walimu na wahadhiri ambao hawajahitimu rasmi katika taaluma ya usoroveya, hali ambayo amesema ni tishio kwa ubora wa elimu nchini.

Nyadimo amesema ni jambo la kusikitisha kuona wanafunzi na wazazi wakitumia fedha nyingi kugharamia elimu ilhali baadhi ya vyuo havina wataalamu wenye sifa zinazohitajika kufundisha taaluma hizo.
“Hatua ya baadhi ya vyuo kutumia wahadhiri ambao hawajahitimu rasmi katika taaluma ya usoroveya ni kuhatarisha mustakabali wa wanafunzi wetu pamoja na kudhoofisha ubora wa taaluma hii muhimu nchini,” amesema Nyadimo.
Amesema endapo hali hiyo haitadhibitiwa mapema, huenda taifa likazalisha wahitimu wasiokuwa na ujuzi wa kutosha kukidhi mahitaji ya soko la ajira pamoja na kutekeleza majukumu yao kwa weledi unaohitajika.
“Kama taifa tunahitaji kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaopitia mafunzo haya wanapata elimu bora inayokidhi mahitaji ya sasa ya soko la ajira na maendeleo ya taifa. Haiwezekani kuzungumzia maendeleo ya miundombinu bila kuwa na wataalamu waliopitia mafunzo bora,” ameongeza.
Aidha, Nyadimo amesema taaluma ya usoroveya ina mchango mkubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo upangaji wa ardhi, ujenzi wa barabara, majengo, reli pamoja na miradi mingine ya maendeleo, hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa wanaoingia katika taaluma hiyo wanapata mafunzo ya kiwango cha juu.
Hata hivyo amevitaka taasisi za kudhibiti elimu nchini kuongeza ukaguzi wa mara kwa mara katika vyuo vinavyotoa taaluma za usoroveya ili kubaini iwapo zina vifaa vya kutosha vya mafunzo pamoja na wahadhiri wenye sifa zinazotakikana kisheria.
“Tunazitaka TVETA na CUE kuhakikisha kila taasisi inayotoa mafunzo ya usoroveya inafuata viwango vilivyowekwa. Hii itasaidia kulinda hadhi ya taaluma yetu pamoja na kuhakikisha wahitimu wetu wanakuwa na ushindani katika soko la ajira,” amesema.
Washikadau waliohudhuria kongamano hilo pia wamejadili changamoto zinazoikumba sekta hiyo pamoja na njia za kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kisasa katika mafunzo na utekelezaji wa kazi za usoroveya nchini.
NA HARRISON KAZUNGU.