Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini imetangaza kuwa hali ya hewa ya mchanganyiko inatarajiwa kushuhudiwa wiki hii katika maeneo mbalimbali ya pwani na sehemu nyingine za nchi.
Kulingana na utabiri huo, mvua zinatarajiwa kunyesha nyakati za asubuhi na mchana katika baadhi ya maeneo ,Viwango vya joto mchana vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 30 hadi 31 za Selsiasi, huku usiku vikishuka hadi takriban nyuzi 24 za Selsiasi.
Aidha, upepo wa wastani hadi mkali kutoka kusini mashariki unatarajiwa kuendelea, sambamba na hali ya bahari ya wastani ambayo inaweza kuwa na mawimbi makali kuelekea mwishoni mwa wiki.
Wavuvi na wananchi wanaofanya shughuli za baharini wametakiwa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuchukua tahadhari kutokana na upepo mkali pamoja na mawimbi yanayoweza kuongezeka.