Waziri wa Leba, Dkt. Alfred Mutua, ameungana na mamia ya vijana pamoja na mawakala wa kampuni za ajira ughaibuni katika kaunti ya Mombasa, kushiriki zoezi la siku tatu la kuwasajili vijana wanaotafuta nafasi za kazi nje ya nchi, katika juhudi za serikali kupunguza ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana nchini.
Akizungumza na wanahabari katika chuo cha kiufundi cha National Industrial Training Authority (NITA), Mutua amesema kuwa serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha vijana wanapata fursa za ajira katika masoko ya kimataifa kwa njia salama na iliyo halali.
“Kuna zaidi ya nafasi 4,000 za kazi ughaibuni. Hii ni fursa muhimu kwa vijana wetu, na ninawahimiza wajitokeze kwa wingi ili kunufaika na nafasi hizi na kuboresha maisha yao pamoja na familia zao,” amesema Mutua.
Ameeleza kuwa sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi, afya, ukarimu na teknolojia zinaendelea kutoa nafasi nyingi za ajira nje ya nchi, huku serikali ikiendelea kushirikiana na washirika wa kimataifa kuhakikisha kuwa ajira hizo zinapatikana kwa njia iliyo wazi na yenye kuzingatia haki za wafanyakazi.
Waziri huyo amesisitiza kuwa serikali imejizatiti kulinda maslahi ya Wakenya wanaoenda kufanya kazi ughaibuni kwa kuhakikisha mikataba ya ajira inazingatia sheria za kazi na haki za binadamu.
Wakati huo huo, Mutua ametoa onyo kali kwa makampuni ya utapeli yanayojifanya kutoa ajira za nje, akisema serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika.
“Kuna baadhi ya kampuni zisizo halali zinazowatapeli wananchi kwa ahadi za ajira nje ya nchi. Serikali kupitia Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imeunda kitengo maalum cha kufuatilia na kuchunguza kampuni hizo ili kuhakikisha wanaohusika wanachukuliwa hatua za kisheria,” amesema Mutua.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya wizara yake na vyombo vya usalama umeimarishwa ili kukomesha vitendo vya ulaghai vinavyowaathiri vijana wengi wanaotafuta ajira.
Aidha, amewataka wanaotafuta ajira kuwa waangalifu na kuchukua hatua za kuthibitisha uhalali wa kampuni kabla ya kujisajili au kutoa malipo yoyote.
“Ni muhimu kwa kila anayetafuta ajira kuthibitisha kampuni kupitia Mamlaka ya Kitaifa ya Ajira (NEA) au kutumia nambari rasmi za uthibitisho. Hii itawasaidia kuepuka kudanganywa na kupoteza fedha zao,” amesema Mutua.
Zoezi hilo la siku tatu linatarajiwa kuvutia maelfu ya vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Pwani na hata kaunti jirani, huku likiwa sehemu ya juhudi za serikali za kufungua milango ya ajira kwa vijana na kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira nchini.
NA HARRISON KAZUNGU.