WANAHABARI WATAKIWA KUPEWA RASILIMALI NA ULINZI IMARA DHIDI YA DHULUMA MIONGONI MWAO MUDI ATOA WITO MOMBASA.
By Dayo Radio
Published on 05/05/2026 10:32 • Updated 05/05/2026 10:40
News

Mwenyekiti wa Baraza la wanahabari kaunti ya Mombasa chini ya Media Council of Kenya (MCK), Maurine Mudi, amewataka wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha wanahabari wanapatiwa rasilimali za kutosha ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari mjini Mombasa, Mudi amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa sera na sheria madhubuti zitakazolinda haki, usalama na maslahi ya wanahabari nchini.

 

Aidha amesema changamoto ya ukosefu wa rasilimali katika baadhi ya vyombo vya habari imekuwa ikikwamisha kazi ya wanahabari na kuathiri ubora wa taarifa zinazowafikia wananchi.

Hata hivyo, Mudi ameonyesha wasiwasi wake kuhusu ongezeko la visa vya dhuluma dhidi ya wanahabari wa jinsia ya kike hususan katika mitandao ya kijamii, hali ambayo amesema imekuwa ikiwakatisha tamaa wengi wao na kuathiri hata nafasi zao za uongozi wanapofikia umri wa miaka 45 na kuendelea.

 

“Ni jambo la kusikitisha kuona wanahabari wanawake wakikumbana na mashambulizi na dhuluma mtandaoni, jambo ambalo linadhoofisha morali yao na nafasi zao za maendeleo ya kikazi,” amesemea Mudi.

Kwa upande wake, katibu mkuu wa muungano wa wanahabari wa Coast Media, Brian Otieno, ametoa wito kwa wadau wa sekta ya habari kuhakikisha wanahabari wanapewa nafasi ya kufanya kazi bila vikwazo ili kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Uhuru wa vyombo vya habari ni msingi muhimu wa demokrasia, hivyo ni lazima wanahabari waachiwe nafasi ya kufanya kazi zao kwa uhuru na usalama,” amesemea Otieno.

Vile vile, mwanaharakati kutoka shirika la Vocal Africa, Nahida Kassim, ameeleza kuwa wataendelea kushirikiana na wanahabari hasa wale wanaokumbana na dhuluma kwa kuwapatia msaada wa kisheria na kijamii ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!