Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza kuwa imefikia asilimia 75 ya lengo la usajili mpya wa wapiga kura nchini, katika zoezi linaloendelea ambalo linatarajiwa kukamilika Jumanne ya leo.
Kwa mujibu wa IEBC, jumla ya wapiga kura wapya milioni 1.87 tayari wamesajiliwa kati ya lengo lililowekwa la milioni 2.5 tangu kuanza kwa zoezi hilo Machi 30 mwaka huu. Tume hiyo imeeleza kuwa mafanikio hayo ni ishara ya mwitikio chanya kutoka kwa wananchi, hasa vijana waliotimiza umri wa kupiga kura.
Aidha, IEBC imesisitiza kuwa katika kipindi cha wiki moja pekee, kati ya Aprili 17 na Aprili 23, zaidi ya wapiga kura 505,000 waliandikishwa, hali inayodhihirisha kuongezeka kwa hamasa ya wananchi kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, kaunti ya Nairobi inaongoza kwa idadi kubwa ya waliojiandikisha, ikifuatiwa na Kiambu, Nakuru, Kakamega, Machakos na Bungoma. Kaunti hizi zimeonekana kuwa na mwitikio mkubwa kutokana na msongamano wa watu na uhamasishaji uliofanywa na wadau mbalimbali.
Hata hivyo, IEBC imebainisha kuwa baadhi ya kaunti zimeendelea kurekodi idadi ndogo ya usajili, ambapo Lamu inaongoza kwa kuwa na idadi ya chini zaidi ya waliojiandikisha, ikifuatwa na Isiolo na Mandera. Tume hiyo imeeleza kuwa inaendelea kuweka mikakati ya ziada ili kuongeza uhamasishaji katika maeneo hayo yenye mwitikio mdogo.
IEBC pia imewahimiza wananchi ambao bado hawajajisajili kujitokeza kwa wingi kabla ya muda wa zoezi hilo kukamilika, ikisisitiza umuhimu wa kila mwananchi mwenye sifa kushiriki katika uchaguzi kwa njia ya kupiga kura.
Vilevile, tume hiyo imesema kuwa huduma za usajili zitaendelea kupatikana hata baada ya kukamilika kwa awamu ya sasa, kupitia vituo vya kutoa huduma, ofisi za IEBC katika maeneo bunge pamoja na makao makuu yake, ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayekosa fursa ya kujiandikisha kama mpiga kura.
IEBC imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha mchakato wa uchaguzi nchini unakuwa huru, haki na wa kuaminika, huku ikiwataka wadau wote kuunga mkono juhudi za kuimarisha demokrasia nchini Kenya.
NA HARRISON KAZUNGU.