Taasisi ya BrighterMonday, taasisi inayojishughulisha na kuunganisha waajiri na watafuta kazi pamoja na kutoa suluhisho za ajira na maendeleo ya ujuzi, kwa ushirikiano na wadau wa sekta ya ulinzi nchini Kenya wameanzisha mpango mpya unaolenga kuimarisha uongozi wa usalama katika mashirika na wakati huo huo kufungua fursa zaidi za ajira kwa vijana nchini.
Mpango huo mpya unalenga si tu kuboresha viwango vya usalama katika mashirika mbalimbali bali pia kuhakikisha kuwa vijana wanapatiwa nafasi za ajira zenye hadhi kupitia mafunzo maalum yanayowaandaa kukabiliana na mahitaji halisi ya soko la ajira. Ushirikiano huo pia unatarajiwa kusaidia kujenga daraja kati ya waajiri na watafuta kazi kwa kutumia mifumo ya kisasa inayozingatia ufanisi, uwazi na matokeo bora.

Akizungumza jijini Nairobi, Kiongozi wa Programu na Mkuu wa Mikakati wa BrighterMonday, Bi. Penina Kimani, amesema kuwa mabadiliko ya kiteknolojia na changamoto mpya za kiusalama zinahitaji mbinu bunifu katika kuajiri na kusimamia rasilimali watu katika sekta hiyo.
“Tunashuhudia mabadiliko makubwa katika sekta ya usalama, ambapo mahitaji ya ujuzi maalum yanaongezeka kila siku. Ni muhimu kwa mashirika kuwekeza katika mifumo bora ya kuajiri na pia kuwajengea vijana uwezo wa kukidhi mahitaji hayo,” amesema Bi. Kimani.
Ameeleza kuwa kupitia ushirikiano huo, vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 35 watanufaika kwa kupata ajira zenye staha pamoja na mafunzo ya kitaaluma na kiufundi yatakayowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi katika sekta ya usalama.
“Lengo letu ni kuhakikisha vijana hawapati tu ajira, bali pia wanapata ujuzi endelevu utakaowawezesha kukua kitaaluma na kuchangia kikamilifu katika uchumi wa nchi,” ameongeza.

Kwa mujibu wa wadau wa sekta hiyo, usalama ni nguzo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi kwani huwezesha uwekezaji, biashara na shughuli nyingine za kijamii kufanyika katika mazingira salama na yenye utulivu. Hivyo, kuimarisha sekta hiyo kunachangia moja kwa moja ustawi wa taifa.
Kupitia mpango wa Gen-Kazi unaotekelezwa kwa ushirikiano na Mastercard Foundation, BrighterMonday inaendelea kutoa mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa vijana, ikiwa ni pamoja na ujuzi wa kiufundi, mawasiliano na utayari wa kazi (employability skills). Mpango huo pia unalenga kuwafikia vijana kutoka makundi mbalimbali wakiwemo wanawake, vijana wa maeneo ya mashinani na watu wanaoishi na ulemavu.
Bi. Kimani amesisitiza kuwa ushirikiano huo utafungua fursa mpya kwa vijana wengi zaidi na kusaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.
“Ushirikiano huu ni hatua kubwa katika juhudi za kuhakikisha hakuna kijana anayebaki nyuma katika suala la ajira. Tunataka kuona vijana wakinufaika na fursa zilizopo na kuwa sehemu ya suluhisho la maendeleo ya taifa,” amesema.
Aidha, ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia katika mchakato wa ajira yatasaidia kuongeza uwazi na ufanisi, huku yakipunguza mianya ya upendeleo au ukosefu wa haki katika upatikanaji wa ajira.
Mpango huo unatarajiwa kuendelea kupanuka katika maeneo mbalimbali nchini, huku ukihusisha wadau zaidi ili kuhakikisha matokeo yake yanafika kwa vijana wengi zaidi.
Kwa ujumla, juhudi hizi zinaashiria dhamira ya pamoja ya wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa vijana wanapatiwa mazingira bora ya kujifunza, kuajirika na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Kenya.
NA HARRISON KAZUNGU.