NACC NA VIONGOZI WA DINI WAUNGANA KUKUZA MAADILI, UMOJA NA MATUMIZI SAHIHI YA MITANDAO YA KIJAMII NCHINI.
By Dayo Radio
Published on 18/04/2026 19:50
News

Muungano wa masuala ya kidini wa National Association of Christian Chaplains (NACC) umehimiza umuhimu wa kudumisha utangamano, mshikamano na matumizi bora ya mitandao ya kijamii kwa heshima, bila kumkosea au kumdhalilisha mtu mwingine.

Muungano huo umeeleza kuwa umeendelea kutoa huduma za kidini katika vyuo mbalimbali nchini, hatua inayolenga kuwajenga wanafunzi kimaadili ili wawe na tabia njema shuleni na hata watakapokuwa viongozi wa baadaye.

Wakizungumza na waandishi wa habari, viongozi hao wamesema kuwa kwa muda mrefu kumekuwepo na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, hali ambayo imeathiri jamii kwa namna mbalimbali, ikiwemo athari za kisaikolojia.

 “Kwa muda mrefu kumekuwepo na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, hali ambayo imeathiri watu wengi kisaikolojia,”

Msemaji wa NACC, John Ngatu, amewataka wananchi kuzingatia nidhamu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, akionya dhidi ya matumizi ya mitandao kwa namna inayoweza kuchochea chuki au migawanyiko.

“Tuwahimize wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa heshima na kwa kujenga amani badala ya kuibua chuki na migawanyiko,” amesema John Ngatu.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Muslim Professionals League Africa, Dkt. Hassan Kinyua Omari, ameahidi kuwa Waislamu wako tayari kushirikiana na NACC katika kuimarisha maadili miongoni mwa vijana.

“Wanafunzi wanapaswa kupewa mafunzo ya dini kwa hiari bila kulazimishwa, ili kuhakikisha hakuna uhasama baina ya dini,” amesema Dkt Hassan Kinyua akisisitiza umuhimu wa kuheshimiana na kuishi kwa amani.

Wakati huo huo, muungano wa NACC umetoa wito kwa serikali kuzingatia maslahi ya viongozi wa kidini wanaoshiriki katika uhamasishaji mashuleni, ukieleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakitoa huduma hizo bila malipo kutokana na mapungufu ya mtaala wa awali.

Muungano huo umesisitiza kuwa kutambuliwa kwa mchango wao na kupewa motisha kutaimarisha zaidi malezi ya kimaadili kwa wanafunzi nchini na kuchangia jamii yenye maadili imara.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!