Ni afueni kwa Wakenya na sekta ya uchukuzi baada ya Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Petroli (EPRA) kutangaza kushuka kwa bei ya mafuta kufuatia marekebisho ya ushuru wa Ongezeko la Thamani (VAT).
Katika taarifa yake, EPRA imesema kuwa ushuru wa VAT umepunguzwa kutoka asilimia 13 hadi asilimia 8, hatua iliyochukuliwa na serikali ya William Ruto kwa lengo la kupunguza gharama ya maisha kwa wananchi na kusaidia sekta mbalimbali za uchumi, hususan usafiri na biashara.
“Tumeamua kupunguza VAT ya mafuta kwa muda ili kupunguza mzigo kwa wananchi na kusaidia kupunguza gharama ya maisha nchini.”
Kwa mujibu wa bei mpya zilizotangazwa, petroli na dizeli zimepungua kwa zaidi ya shilingi tisa na kumi kwa kila lita mtawalia, huku bei ya mafuta ya taa ikibaki bila mabadiliko. Mabadiliko haya yanatarajiwa kupunguza gharama za usafiri wa umma, mizigo, pamoja na gharama za uzalishaji viwandani.
Katika jiji la Nairobi, petroli sasa inauzwa kwa shilingi 197.60 kwa lita, dizeli shilingi 196.63, na mafuta ya taa shilingi 152.78. Mjini Mombasa, petroli ni shilingi 194.32, dizeli shilingi 193.35, na mafuta ya taa shilingi 149.49 kwa lita.
Wadau wa sekta ya uchukuzi wamesema hatua hiyo ni nafuu ya muda mfupi inayoweza kusaidia kupunguza nauli za abiria na gharama za usafirishaji wa bidhaa, ingawa wameeleza kuwa bei za mafuta bado zinaendelea kuwa juu kutokana na mabadiliko ya soko la kimataifa na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kenya.
Wachumi pia wamesema kuwa athari kamili ya punguzo hilo inaweza kuchukua muda kuonekana kwa wananchi wa kawaida, kwani baadhi ya makampuni ya usafirishaji na biashara huenda yakachukua muda kurekebisha bei zao.
Hata hivyo, hatua ya kupunguza VAT kwa muda wa miezi mitatu imeelezwa kama mkakati wa serikali wa kutoa unafuu wa haraka kwa wananchi wakati ikiendelea kutafuta suluhu za kudumu za kupunguza mfumuko wa bei na gharama za maisha nchini.
NA HARRISON KAZUNGU.