Wakazi wa maeneo ya Ziwa la Ng’ombe na Mkomani katika eneo bunge la Nyali, kaunti ya Mombasa, wamejumuika pamoja na washikadau mbalimbali wakiwemo mashirika ya kijamii kujadili mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto ya mafuriko ambayo imekuwa ikijirudia kila msimu wa mvua.
Kongamano hilo huo limelenga kutafuta suluhu la kudumu ili kupunguza athari zinazowakumba wakazi kila mwaka.
Kwa mujibu wa wakazi hao, moja ya sababu kuu inayochangia mafuriko hayo ni mipangilio duni ya ujenzi, hasa ujenzi unaofanyika katika mikondo ya maji na maeneo yaliyotengwa kwa mifereji ya kupitisha maji ya mvua.
Hata hivyo wameitaja hali hiyo kama iliyozidisha tatizo hilo na kusababisha hasara kubwa ikiwemo uharibifu wa makazi, mali, na hata kuhatarisha maisha yao.

Aidha, wameeleza kuwa mafuriko hayo hupelekea kuchipuka kwa milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu na malaria kutokana na maji yaliyotuama.
“Mafuriko haya yanatuathiri sana kila mwaka. Tunapoteza mali, watoto wanashindwa kwenda shule, na hata kupata huduma za afya inakuwa changamoto kubwa hasa kwa wazee na watu wanaoishi na ulemavu. Tunaiomba serikali na washikadau kuchukua hatua za haraka kudhibiti ujenzi holela na kuboresha mifereji ya maji.” wamesema wakazi.
Wakati huohuo wakazi hao wamebainisha kuwa watu wanaoishi na ulemavu huathirika zaidi wakati wa mafuriko kwani hupata ugumu wa kufikia huduma muhimu kama hospitali, shule na maeneo ya kujipatia mahitaji ya kila siku.
Kauli hiyo imeungwa mkono na chifu wa lokesheni ya Maweni, Benard Omollo, ambaye amewahimiza wakazi kuwa makini na kuzingatia tahadhari zote zinazotolewa na idara za hali ya hewa ili kujikinga dhidi ya athari za mafuriko.
“Ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha anazingatia maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika. Taarifa za hali ya hewa zinapotolewa, ni muhimu kuzifuatilia na kuchukua hatua mapema ili kulinda maisha na mali.” Amesema chifu Omollo.

Kwa upande wao, wawakilishi kutoka shirika la Dream Achievers Youth Organization (DAYO) akiwemo msimamizi wa miradi anayehusika na masuala ya hali ya anga Linda Indimuli pamoja na mratibu wa programu Enos Opiyo, wamesema kuwa kupitia vikao hivyo wameweza kukusanya maoni kutoka kwa jamii kuhusu mbinu bora za kukabiliana na mafuriko.
Wamesema kuwa jamii imeonyesha utayari wa kushirikiana na mashirika na serikali katika kutekeleza suluhisho, ikiwemo kuhamasisha ujenzi unaofuata sheria, usafi wa mazingira, na matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa wakati.
Aidha, wameongeza kuwa kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kutafsiri na kutumia taarifa za hali ya anga ili kujikinga mapema dhidi ya majanga kama mafuriko.
Kwa ujumla, wadau wote waliohudhuria mkutano huo walikubaliana kuwa ushirikiano kati ya jamii, serikali na mashirika ya kijamii ni muhimu katika kutafuta suluhisho la kudumu la tatizo la mafuriko katika eneo la Nyali na maeneo mengine yanayokumbwa na changamoto kama hiyo.
NA HARRISON KAZUNGU.