Mbunge wa Nyali, Mohamed Ali, amelalamikia kuondolewa kwa mabango yaliyokuwa yakihamasisha wananchi kujisajili kama wapiga kura katika Kaunti ya Mombasa.
Mbunge huyo amesema mabango matatu yaliyokuwa yamewekwa katika maeneo ya Buxton, Ferry na Kibarani yaliondolewa usiku wa Aprili 6 na kudai kuwa hatua hiyo ilifanyika kwa vitisho dhidi ya kampuni za matangazo.
Mbunge huyo Amesisitiza kuwa mabango hayo yalikuwa na ujumbe Kwa wananchi wa kuhamasisha usajili wa wapiga kura, na si wa kisiasa, akiongeza kuwa yalikuwa yamewekwa kihalali kupitia wahudumu walioidhinishwa.
Aidha ameishutumu serikali ya kaunti kwa kile alichokitaja kuwa ni ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza na haki ya wananchi kushiriki katika demokrasia na kuitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, kuingilia kati na kuchunguza tukio hilo.
Hata hivyo, maafisa wa kaunti ya Mombasa wamekanusha kuhusika Kwa kuondolewa kwa mabango hayo.