Ni pigo kubwa kwa mfungwa Daniel Njihia Miano, ambaye alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 14 gerezani kwa kosa la wizi wa kutumia nguvu, baada ya mahakama ya rufaa kumhukumu kifo akiwa amesalia na takriban mwaka mmoja tu kukamilisha kifungo chake. Uamuzi huo umeibua mjadala mpana kuhusu utekelezaji wa adhabu kali kwa makosa ya jinai, hasa pale ambapo mfungwa amekuwa akikaribia kuhitimisha kifungo chake.
Katika uamuzi uliotolewa tarehe 25 Machi 2026 katika mahakama ya rufaa mjini Nakuru, jopo la majaji watatu walitupilia mbali rufaa ya Miano, wakisisitiza kuwa adhabu ya kifo imeainishwa wazi chini ya sheria za Kenya kwa kosa la wizi wa kutumia nguvu, na hivyo haiwezi kubadilishwa katika hatua ya rufaa ya pili.
Majaji hao walieleza kuwa jukumu la mahakama ni kutafsiri na kutekeleza sheria kama ilivyo, bila kuathiriwa na hisia au mazingira binafsi ya mshtakiwa. Waliongeza kuwa mara tu mahakama ya chini inapotoa hukumu inayozingatia sheria, mahakama ya juu haina mamlaka ya kuibadilisha isipokuwa kama kuna dosari ya kisheria au ukiukwaji wa haki za msingi, jambo ambalo halikuthibitishwa katika kesi hiyo.
Kesi hiyo ilitokana na tukio la mwaka 2010 ambapo Miano, kwa kushirikiana na wenzake watatu, alimshambulia mwathiriwa na kumpora simu ya mkononi pamoja na pesa taslimu. Tukio hilo liliripotiwa kwa polisi na baadaye watuhumiwa wakakamatwa na kufikishwa mahakamani, ambapo walipatikana na hatia ya wizi wa kutumia nguvu kosa ambalo kwa mujibu wa sheria linabeba adhabu ya kifo.
Awali, Miano alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 14 gerezani, lakini baada ya mchakato wa rufaa kupitia mahakama mbalimbali, hatimaye hukumu hiyo ilibadilishwa na kuwa adhabu ya kifo kufuatia tafsiri ya kisheria iliyotolewa na mahakama ya rufaa.
Mahakama imeweka wazi kuwa haina mamlaka ya kuingilia adhabu ambayo tayari imeainishwa kisheria, ikisisitiza kuwa mabadiliko yoyote kuhusu adhabu kama hiyo yanapaswa kufanywa kupitia bunge au marekebisho ya sheria, na si kupitia mahakama.
Kisa hiki kinaendelea kuibua hisia miongoni mwa wananchi na wadau wa haki za binadamu, huku wengine wakitaka marekebisho ya sheria ili kuzingatia hali na mazingira ya wahalifu kabla ya kutoa adhabu kali kama ya kifo.
NA HARRISON KAZUNGU.