Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kurunzi Cerebral Palsy, Mwanaisha Mohamed, amewasihi wazazi na jamii kwa ujumla kuwapa malezi bora watoto wenye ulemavu wa akili na kuachana kabisa na vitendo vya unyanyapaa vinavyowanyima haki zao za msingi.
Akizungumza katika hafla ya kuwafanyia ukaguzi watoto wenye ulemavu wa akili iliyofanyika katika Zahanati ya Ziwa la Ng’ombe, Mombasa, Mwanaisha ameeleza kuwa kila mtoto ana ndoto na matarajio yake maishani, hivyo ni wajibu wa jamii kuhakikisha wanapatiwa mazingira bora ya kuzitimiza ndoto hizo sawa na watoto wengine.
“Kila mtoto ana ndoto zake na ana haki ya kuzipata. Jamii inapaswa kuwapa nafasi sawa kama watoto wengine na kuacha kabisa unyanyapaa,” amesema Mwanaisha Mohamed.
Amesisitiza kuwa watoto wenye ulemavu wanahitaji upendo, uelewa na msaada wa karibu kutoka kwa familia na jamii ili waweze kukuza vipaji vyao na kujiamini. Ameongeza kuwa kuwaficha watoto hao au kuwanyanyapaa ni kinyume na haki za binadamu na kunadumaza maendeleo yao kijamii na kiakili.

Hafla hiyo imewaleta pamoja wahisani na mashirika mbalimbali ya kijamii, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za afya na ustawi kwa watoto wenye mahitaji maalum katika jamii.
Kwa upande wake, mmoja wa wazazi, Melyn Andisi, amesifia hatua hiyo akieleza kuwa imeleta manufaa makubwa kwa watoto hao pamoja na familia zao. Amesema kuwa huduma kama hizi zinawapa matumaini na mwanga wa maisha bora zaidi.
“Tusifiche watoto wetu wenye ulemavu, kufanya hivyo ni kuwanyima haki zao za msingi na nafasi ya kuishi maisha yenye heshima,” amesema Melyn Andisi.
Aidha, amewasihi wazazi kuacha kuwaficha watoto wenye ulemavu wa akili, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata huduma, elimu na kushirikishwa kikamilifu katika jamii.
Hata hivyo, wito umetolewa kwa wadau mbalimbali kushirikiana katika kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata ulinzi, heshima na fursa sawa kama watoto wengine katika jamii.
NA HARRISON KAZUNGU.