Viongozi wakuu wa kaunti ya Lamu, waziri wa masuala ya sanaa na utamaduni, Dkt. Ruth D Masha wa kaunti ya Kilifi, na Sabrina Mkare Jefwa kutoka idara ya uvuvi, uchumi wa bahari na mifugo, wamehudhuria hafla ya kuapishwa kwa viongozi wapya wa baraza la vijana Kaunti ya Kilifi.
Tukio hilo limeashiria hatua muhimu katika kuimarisha uongozi wa vijana katika eneo kaunti hiyo.

Baraza hilo limeongozwa na rais wake, Felix Balozi, pamoja na viongozi wengine waliochaguliwa, ambao wamejitolea kusukuma mbele maslahi na ustawi wa vijana wa Kilifi. Kuapishwa kwao kunaashiria mwanzo wa juhudi mpya za kuendeleza ajenda za vijana na kuhakikisha maendeleo jumuishi katika jamii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Masha amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji miongoni mwa viongozi hao vijana, huku akiongeza kuwa ni kupitia ushirikiano dhabiti ambapo vijana hao wataweza kufaulu katika safari zao za uongozi.
“Uongozi ni dhamana. Vijana mliopata nafasi hii mnapaswa kuonyesha uadilifu, kujituma na kuwa mfano bora kwa wenzao,” amesema Waziri wa Masuala ya Sanaa, Dkt. Masha.
Kwa upande wake, Sabrina Mkare Jefwa amewahimiza viongozi hao kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya katika jamii.
“Chukueni jukumu hili kwa uzito unaostahili. Simamieni masuala ya vijana kwa ujasiri na hakikisheni sauti zao zinasikika katika ngazi zote za maamuzi,” amesema Sabrina.
Viongozi hao pia wameongeza kuwa uongozi bora katika ngazi ya vijana ni msingi muhimu wa kujenga mustakabali mzuri wa Kaunti ya Kilifi, huku wakiwataka viongozi wapya kushirikiana, kudumisha umoja na kubaki waaminifu katika kuwahudumia vijana wenzao.
Hafla hiyo imepokelewa vyema na washiriki mbalimbali, wengi wakieleza matumaini yao kwamba uongozi mpya utaleta mabadiliko chanya na fursa zaidi kwa vijana wa Kilifi.
NA HARRISON KAZUNGU.