MURKOMEN AMLIPUA TUJU KWA “UTEKAJI BANDIA”, AMTAKA MAHAKAMA KUCHUKUA HATUA KALI.
By Dayo Radio
Published on 24/03/2026 14:36
News

Waziri wa usalama wa ndani, Kipchumba Murkomen, amemshutumu vikali aliyekuwa Waziri, Raphael Tuju, kwa kile alichodai kuwa ni kupanga tukio la kutoweka kwake kwa lengo la kujipatia huruma ya umma.

Murkomen amesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa Tuju hakuwa ametoka nyumbani kwake katika eneo la Karen wakati familia yake iliporipoti kutoweka kwake, akieleza kuwa dalili zote zinaonyesha alikuwa bado ndani ya makazi hayo.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha wazi kuwa mhusika hakuondoka nyumbani kwake. Simu yake imepatikana ndani ya chumba chake, jambo linalotia shaka kubwa madai ya kutoweka kwake,” amesema Murkomen.

Ameongeza kuwa maafisa wa upelelezi wamefanikiwa kufuatilia simu ya Tuju hadi ndani ya chumba chake, huku akidai kuwa familia ilionyesha kusitasita na hata kukataa awali kuruhusu maafisa wa polisi kuingia ndani ya nyumba hiyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, tukio hilo linaashiria uwezekano wa mpango uliolenga kupotosha umma na kuibua hisia za huruma, hali ambayo amesema ni hatari kwa usalama wa taifa na uaminifu wa taasisi za dola.

“Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya watu wakijaribu kupotosha umma kwa kupanga visa vya utekaji bandia. Matukio kama haya yanapunguza uzito wa matukio halisi ya uhalifu na kuathiri juhudi za vyombo vya usalama,” ameongeza Murkomen.

Murkomen amesisitiza kuwa serikali haitavumilia vitendo vya aina hiyo, akionya kuwa yeyote atakayepatikana na hatia atakabiliwa na mkono wa sheria bila upendeleo.

“Serikali iko imara katika kuhakikisha sheria inafuatwa. Hakuna atakayekuwa juu ya sheria, na tutahakikisha wahusika wanawajibishwa ipasavyo,” amesema.

Aidha, Waziri huyo ameitaka mahakama kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaopanga visa vya utekaji bandia, akisema kuwa adhabu kali itasaidia kutoa funzo kwa wengine wanaoweza kuwa na nia kama hiyo.

“Tunaiomba mahakama ichukue hatua kali na za haraka dhidi ya wahusika wa matukio kama haya ili kulinda uadilifu wa mfumo wetu wa haki na kurejesha imani ya wananchi kwa vyombo vya usalama,” amesisitiza.

Kauli hiyo imeibua mjadala mpana miongoni mwa wananchi, huku baadhi wakitaka uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini ukweli kamili wa tukio hilo, na wengine wakisisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika masuala yanayohusu usalama wa raia.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!