KAMATI YA AFYA BUNGENI YAWATAKA WAKENYA KULIPA ADA ZA SHA HUKU IKIONYA KUHUSU MZIGO MKUBWA UNAO ATHIRI HUDUMA ZA AFYA.
By Dayo Radio
Published on 19/03/2026 17:16
News

Kamati ya Bunge kuhusu Afya imewataka Wakenya kuhakikisha wanalipa ada za Social Health Authority (SHA) ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini.Akizungumza baada ya kikao cha kamati hiyo, Mwenyekiti wake, Dr. James Nyikal, amesema kuwa licha ya hatua kubwa iliyofikiwa katika usajili wa wananchi, bado kuna changamoto kubwa katika ulipaji wa ada za kila mwezi.

Nyikal amesema kuwa zaidi ya Wakenya milioni 29 tayari wamejisajili katika mpango huo, lakini ni watu milioni 5 pekee wanaotekeleza wajibu wa kulipa ada hizo kila mwezi, hali ambayo imeendelea kuuweka mfumo huo katika hatari ya kulemewa.

“Tuna wakenya milioni 29 ambao wameshajisajili kwa SHA, lakini ni watu milioni 5 pekee wanaolipa ada kila mwezi. Hii inaweka mzigo mkubwa kwa mfumo wa huduma za afya na kuathiri uendelevu wake,” amesema Nyikal.

Ameongeza kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha wananchi wengi kukumbana na changamoto wanapohitaji huduma za matibabu, huku baadhi yao wakilazimika kugharamia bili za hospitali kwa fedha zao binafsi kutokana na ucheleweshaji au ukosefu wa huduma kupitia SHA.

“Wachache wanaolipa hawawezi kubeba gharama za huduma kwa idadi kubwa ya Wakenya. Ni muhimu kila anayestahili ajitokeze na kulipa ili kuhakikisha mfumo huu unafanya kazi kwa ufanisi,” amesisitiza.

Wakati huo huo, kamati hiyo imebaini kuwa changamoto za kiutendaji ndani ya SHA pia zinachangia ucheleweshaji wa huduma, hasa katika mchakato wa kidijitali ambao bado haujakamilika kikamilifu.

Kutokana na hali hiyo, kamati imependekeza hatua za haraka kuchukuliwa ili kuboresha utendaji wa mamlaka hiyo, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wafanyakazi na kuimarisha miundombinu ya kiteknolojia.

“Tumeishauri SHA kuajiri wahudumu zaidi na kuharakisha uhamiaji wa mfumo wa kidijitali. Hii itarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na kupunguza malalamiko yanayoendelea kushuhudiwa,” amesema Nyikal.

Kamati hiyo imehimiza pia kuwepo kwa kampeni za uhamasishaji kwa umma ili kuwahamasisha Wakenya kuelewa umuhimu wa kuchangia katika mfuko huo wa afya, ikisisitiza kuwa mafanikio ya SHA yanategemea ushiriki wa kila mwananchi.

Kwa sasa, kamati inaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mapendekezo hayo ili kuhakikisha mfumo wa SHA unakuwa thabiti na wenye uwezo wa kuwahudumia wakenya wote kwa haki na usawa.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!