Aliyekuwa Mbunge wa Kisauni, Ali Menza Mbogo, amesema kuwa viongozi wa kaunti ya Mombasa wameanza safari ya mageuzi ya kisiasa yenye lengo la kuimarisha uongozi, kuboresha utoaji wa huduma na kurejesha matumaini ya wananchi.
Mbogo amesema haya baada ya kuhudhuria mkutano wa mashauriano ya ngazi ya juu ulioitishwa na Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA),Hassan Omar Hassan, uliowakutanisha viongozi mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya kaunti ya Mombasa.

Amesema kikao hicho kimekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana mawazo, kutathmini hali halisi ya kisiasa na kijamii, pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha chama na kushughulikia changamoto zinazowakumba wananchi.
“Tumekuwa na kikao chenye tija kubwa kilichojaa mijadala ya wazi, tathmini ya kina na maamuzi ya busara kuhusu mustakabali wa Mombasa. Hii siyo mikutano ya kawaida, bali ni hatua ya mwanzo ya mageuzi tunayoyakusudia,” amesema Mbogo.h

Katika mkutano huo, Mbogo amesema viongozi hao wameonyesha mshikamano mkubwa na dhamira ya pamoja ya kuhakikisha kuwa chama kinaendelea kuwa imara katika eneo hilo huku kikijikita zaidi katika mahitaji ya wananchi wa kawaida.
Ameeleza kuwa viongozi hao pia wamethibitisha uungwaji mkono wao kwa serikali ya Rais William Ruto, wakisema kuwa ajenda ya maendeleo ya kitaifa ni muhimu kwa ustawi wa wananchi wote, wakiwemo wa Mombasa.
“Tunathibitisha tena kuwa tuko bega kwa bega na Rais William Ruto katika kuhakikisha ajenda ya maendeleo inafikia wananchi wote bila ubaguzi. Hata hivyo, maendeleo hayo lazima yaonekane pia katika ngazi ya kaunti,” ameongeza.

Hata hivyo, Mbogo amesema kuwa pamoja na uungwaji mkono huo, viongozi hao wameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya uongozi katika kaunti ya Mombasa, akibainisha kuwa wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa huduma bora, uwajibikaji mdogo na kutotekelezwa kwa ahadi walizopewa.
“Ujumbe kutoka kwa wananchi uko wazi kabisa wanataka kuona mabadiliko ya kweli. Wanataka huduma bora, uongozi unaosikiliza kilio chao na uwajibikaji wa dhati. Hatuwezi kupuuza sauti hiyo,” amesema.
Mbogo ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo, viongozi hao wameanza mikakati ya kujipanga kisiasa kwa lengo la kutoa mbadala bora wa uongozi utakaojikita katika maslahi ya wananchi.
“Safari ya mabadiliko imeanza rasmi. Tunajipanga upya, tunahamasisha wananchi mashinani na tunaandaa uongozi mpya utakaojikita katika uwazi, uwajibikaji na huduma kwa wananchi,” amesisitiza.
Aidha, amesema kuwa mkakati huo utahusisha kushirikisha vijana, wanawake na makundi yote ya kijamii ili kuhakikisha kuwa kila sauti inawakilishwa ipasavyo katika uongozi wa baadaye.
“Tunataka kujenga uongozi unaowajumuisha wote—vijana, kina mama na makundi yote ya jamii. Huu siyo wakati wa ubaguzi bali ni wakati wa umoja na ushirikiano,” amesema.
Mbogo amesisitiza kuwa nguvu ya mabadiliko iko mikononi mwa wananchi wenyewe, akiwataka kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kisiasa na kufanya maamuzi sahihi yatakayobadilisha mustakabali wa kaunti hiyo.
“Mabadiliko ya kweli huanza na wananchi. Tunawaomba waendelee kuwa sehemu ya safari hii kwa kujitokeza, kushiriki na kusimamia mustakabali wao,” ameongeza.
Katika hitimisho lake, Mbogo amesema kuwa viongozi hao wameazimia kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha kuwa malengo waliyojiwekea yanatimia na kwamba Mombasa inapata uongozi unaostahili.
“Mwelekeo wetu ni mmoja umoja, uwezeshaji wa wananchi na uongozi unaoakisi matarajio halisi ya watu wa Mombasa. Tunaamini kuwa kwa pamoja, tunaweza kuandika ukurasa mpya wa historia ya kaunti hii,” amemalizia.
NA HARRISON KAZUNGU.