Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ameagiza kuundwa kwa jopo maalum ndani ya saa 48 ili kutathmini uharibifu uliosababishwa na mafuriko ya mvua kubwa jijini Nairobi.
Sakaja ametoa agizo hilo katika kikao maalum kilichofanyoka jijini humo na kuhudhuriwa na makatibu kutoka idara mbalimbali za serikali ya kaunti kwa lengo la kutathmini athari za mafuriko yaliyoshuhudiwa katika maeneo kadhaa ya jiji.
“Hatuna budi kuchukua hatua za haraka ili kuelewa ukubwa wa uharibifu uliosababishwa na mafuriko jijini Nairobi. Ndani ya saa 48 jopo maalum litakuwa limeundwa kutathmini barabara zilizoathirika, gharama za ukarabati na kutambua maeneo hatarishi, huku tukitumia teknolojia za Google na ESRI kutengeneza ramani sahihi za mafuriko,” amesema Johnson Sakaja.

Katika kikao hicho, kamati ya utekelezaji imeagiza kuhusishwa kwa mashirika ya barabara nchini ikiwemo Kenya Urban Roads Authority (KURA), Kenya National Highways Authority (KeNHA) na Kenya Rural Roads Authority (KeRRA) ili kutathmini barabara zilizoathirika pamoja na kukadiria gharama za ukarabati.
Aidha, kikao hicho kimekubaliana kutumia teknolojia za kampuni ya Google pamoja na mfumo wa ramani wa Esri ili kutengeneza ramani sahihi za maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko na kusaidia kupanga mikakati ya kudhibiti majanga kama hayo siku zijazo.

Hatua hiyo inajiri baada ya wizara ya ndani kunakili vifo vya watu 66 kufuatia mafuriko yanayoendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini, huku mitaa 37 ikitajwa kuwa hatarini kukumbwa na mafuriko, yakiwemo majengo yaliyojengwa kando ya Mto Nairobi.
NA HARRISON KAZUNGU.