Shirika la vijana la Dream Achievers Youth Organization Kenya (DAYO) limewashauri wakazi wa Mombasa kutozipuuza taarifa na tahadhari zinazotolewa na idara zinazohusika na usimamizi wa majanga.
Afisa wa Mradi wa DARAJA kutoka shirika la DAYO, Bi. Linda Indimuli,alitaja Maeneo ya Bangladesh (Jomvu), Kalahari (Changamwe), Utange na Junda (Kisauni) pamoja na Ziwa la Ng’ombe na Maweni kuwa miongoni mwa maeneo yaliyo katika hatari kubwa ya kuathiriwa na mafuriko katika Kaunti ya Mombasa.

Wakati huo huo, Serikali ya Kaunti ya Mombasa kupitia kitengo cha usimamizi wa majanga imewaonya wakazi wa kaunti hiyo dhidi ya kutupa taka ovyo na kuziba mifereji ya maji hasa katika kipindi hiki cha mvua.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Majanga, Ibrahim Basafar, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayepatikana na hatia ya kuziba mifereji ya maji kwa kutupa taka, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinahatarisha maisha ya wananchi endapo mafuriko yatatokea.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Eneo Bunge la Nyali, Timothy Tirop, amewahimiza wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni kuhamia sehemu salama ili kuepuka hatari ya mafuriko pindi mvua itakapoanza kunyesha.

Viongozi hao walikuwa wakizungumza wakati wa kikao kilichowakutanisha maafisa wa usalama wa kitaifa, wataalamu kutoka Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya, maafisa wa Serikali ya Kaunti ya Mombasa pamoja na mashirika ya kijamii.

Mwisho.