Serikali imekanusha madai yanayosambazwa mitandaoni kuhusu kile kinachodaiwa kuwa uvamizi au uharibifu wa Karura Forest, ikisema kuwa taarifa hizo ni za kupotosha umma na hazina msingi wowote wa ukweli.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura amesema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakieneza habari zisizo sahihi kuhusu kinachoendelea katika eneo hilo, jambo ambalo linaweza kusababisha taharuki miongoni mwa wananchi.
Dkt. Mwaura amesema kuwa serikali imebaini kuwa baadhi ya taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii zinajaribu kuonyesha kana kwamba kuna ukataji mkubwa wa miti au uvamizi wa msitu huo, jambo ambalo amesisitiza kuwa si la kweli.

“Kuna watu wamekuwa wakijaribu kutilia chumvi na kupotosha umma kuhusu kinachofanyika katika Msitu wa Karura. Taarifa hizi si sahihi na zina lengo la kupotosha wananchi,” amesema.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa serikali, ardhi inayotumika katika shughuli zinazozungumziwa ni sehemu ndogo tu ya eneo hilo ambayo tayari ilikuwa imetengwa kwa ajili ya shughuli maalum za utafiti wa miti.
Ameeleza kuwa ardhi hiyo ni takribani ekari tatu pekee na ni sehemu ya kitalu cha miti kinachosimamiwa na Tree Biotechnology Programme Trust.
“Ardhi itakayotumika ni ekari tatu pekee, na tayari ilikuwa imetengwa kwa ajili ya kitalu cha Tree Biotechnology Programme Trust. Hii si ardhi mpya wala hakuna sehemu ya msitu inayosafishwa kwa ajili ya shughuli mpya,” amefafanua.
Dkt. Mwaura amesisitiza kuwa shughuli zinazoendelea katika eneo hilo hazihusishi ukataji mpya wa miti wala uharibifu wa mazingira, bali ni ukarabati wa miundombinu iliyokuwepo awali katika eneo hilo.
“Kinachofanyika ni ukarabati wa miundombinu katika ardhi ambayo tayari ilikuwa imetengwa kwa ajili ya kitalu hicho cha miti. Hakuna ukataji mpya wa miti wala uharibifu wa msitu wa Karura,” ameongeza.
Aidha, msemaji huyo wa serikali amesema kuwa serikali inaendelea kujitolea kulinda misitu na mazingira ya nchi, akibainisha kuwa msitu wa Karura ni moja ya maeneo muhimu ya uhifadhi wa mazingira nchini.
Amesema serikali haitaruhusu hatua yoyote ambayo inaweza kuhatarisha uhifadhi wa mazingira au kuathiri rasilimali za asili zinazotegemewa na wananchi.
Dkt. Mwaura amewahimiza wananchi kuwa makini na taarifa wanazopokea hasa kupitia mitandao ya kijamii, akiwataka kuthibitisha ukweli wake kabla ya kuzisambaza.
“Tunawasihi wananchi kupuuza taarifa zisizo sahihi na badala yake kutegemea taarifa rasmi kutoka kwa mamlaka husika ili kuepuka upotoshaji,” amesema.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea kutoa ufafanuzi pale inapobidi ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu masuala yanayohusu rasilimali za umma na mazingira.
NA HARRISON KAZUNGU.