WADAU WA SEKTA YA UCHUKUZI WAELEZA WASIWASI KUHUSU MFUMO MPYA WA FAINI ZA PAPO KWA HAPO WA NTSA.
By Dayo Radio
Published on 11/03/2026 08:53
News

Washikadau katika sekta ya uchukuzi nchini wameonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu utekelezaji wa mfumo mpya wa faini za papo kwa hapo unaotekelezwa na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani (NTSA).

Washikadau hao wanasema wanahofia kwamba madereva wanaweza kupokea faini zisizo sahihi kutokana na makosa ya mfumo au upungufu wa taarifa.

Akizungumza kwa niaba ya wadau hao, mmoja wa wahudumu katika sekta hiyo amesema:

“Tunahofia kuwa baadhi ya madereva wanaweza kupokea faini zisizo sahihi kutokana na makosa ya mfumo au ukosefu wa taarifa sahihi. Ni muhimu kwa NTSA kutoa elimu ya kutosha kwa madereva kuhusu makosa yanayotozwa faini na namna mfumo unavyofanya kazi.”

Aidha, wameitaka NTSA kutoa maelekezo na elimu ya kutosha kwa madereva kuhusu makosa yanayopigwa faini, jinsi mfumo unavyofanya kazi na namna ya kupinga faini kabla ya kulipa.

Wadau hao pia wameitaka mamlaka hiyo kuhakikisha kamera za trafiki zinaonekana wazi barabarani ili kuongeza uwazi na kuwasaidia madereva kuwa waangalifu zaidi wanapoendesha magari yao.

“Ni muhimu pia kamera za trafiki ziwekwe wazi barabarani ili kuongeza uwazi na kuhakikisha madereva wanakuwa na tahadhari wanapoendesha.”

Vile vile, wahudumu hao wamependekeza kufanyika kwa mkutano wa haraka kati ya NTSA, polisi na wadau wote katika sekta ya uchukuzi ili kufafanua masuala yote ya utekelezaji wa mfumo huo kabla ya kukamilika.

“Tunapendekeza kuwepo kwa mkutano wa haraka kati ya NTSA, polisi na wadau wote wa sekta ya uchukuzi ili kufafanua masuala yote ya utekelezaji kabla mfumo huu haujakamilika,” amesema mmoja wa wadau hao.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!