SERIKALI YAEKA MSIMAMO MKALI DHIDI YA UFISADI, YAKANUSHA MADAI YA UPOTEVU WA RASILIMALI ZA UMMA.
By Dayo Radio
Published on 10/02/2026 17:02
News

Msemaji wa serikali, Dkt . Isaac Mwaura, amekanusha vikali madai yanayosambazwa mitandaoni na kupitia baadhi ya vyombo vya habari kwamba serikali inapoteza rasilimali nyingi za umma kutokana na vitendo vya ufisadi.

 

Akizungumza mapema leo wakati wa kikao na wanahabari jijini Nairobi, Dkt. Mwaura amesema madai hayo hayana msingi na yanalenga kupotosha umma, akisisitiza kuwa serikali ya Kenya imeweka mikakati thabiti ya kuhakikisha uwajibikaji, uwazi na matumizi bora ya rasilimali za wananchi.

 

“Serikali haitapoteza hata shilingi moja ya fedha za umma kupitia ufisadi. Tumeweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na uwajibikaji ili kuhakikisha kila rasilimali inatumika kwa manufaa ya Wakenya,” amesema Dkt. Mwaura.

Mwaura aidha ameeleza kuwa serikali imesimama kidete katika vita dhidi ya ufisadi, huku akibainisha kuwa hatua kali zimechukuliwa dhidi ya maafisa wa umma waliobainika kuhusika na vitendo vya ufisadi, wakiwemo wakuu wa mashirika ya serikali.

 

“Tumeshuhudia maafisa kadhaa wa ngazi za juu wakilazimishwa kuondoka ofisini baada ya kubainika kuhusika na visa vya ufisadi. Hii ni ishara tosha kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria,” ameongeza.

 

Aidha, Dkt. Mwaura amepongeza hatua ya serikali ya kuanzisha na kuimarisha mifumo ya kidijitali ya malipo katika utoaji wa huduma kwa Wakenya, ikiwemo mfumo wa e-Citizen, akieleza kuwa mfumo huo umesaidia pakubwa kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti mianya ya ufisadi.

 

“Mifumo ya kidijitali kama e-Citizen imeleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma. Imeongeza uwazi, imeimarisha ufanisi na kusaidia kuziba mianya iliyokuwa ikitumiwa vibaya kupoteza fedha za umma,” alisema.

 

Kwa mujibu wa Msemaji huyo, serikali itaendelea kuwekeza katika teknolojia na mifumo ya kisasa ili kuhakikisha huduma kwa wananchi zinatolewa kwa njia iliyo wazi, ya haraka na isiyo na mianya ya ufisadi.

 

“Dira ya serikali ni kujenga utamaduni wa uwajibikaji na uadilifu katika sekta ya umma, na hili litawezekana tu kwa ushirikiano kati ya serikali na wananchi,” amesisitiza.

 

Dkt. Mwaura amewataka wananchi kuwa waangalifu dhidi ya taarifa zisizothibitishwa, na badala yake washirikiane na vyombo husika kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kupambana na ufisadi na kulinda rasilimali za taifa.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!