SERIKALI YAZINDUA RASMI SERA YA E-MOBILITY KULINDA MAZINGIRA NA KUBADILISHA MFUMO WA UCHUKUZI NCHINI
By Dayo Radio
Published on 03/02/2026 15:33
News

Serikali imezindua rasmi sera ya E-Mobility inayolenga kuhamasisha matumizi ya magari ya uchukuzi wa umma na pikipiki zinazotumia umeme badala ya mafuta ya petroli, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuimarisha matumizi ya teknolojia safi katika sekta ya uchukuzi.

Uzinduzi wa sera hiyo unaashiria hatua muhimu ya serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hasa uchafuzi wa hewa unaotokana na matumizi ya mafuta ya petroli katika vyombo vya usafiri.

Aidha ama ametaja kuwa kupitia sera hii, serikali inalenga kuhakikisha sekta ya uchukuzi inaendana na maendeleo ya teknolojia ya kisasa huku ikichangia ukuaji wa uchumi endelevu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, waziri wa uchukuzi Davis Chirchir amesema sera ya E-Mobility ni nyenzo muhimu katika kulinda mazingira na kuboresha maisha ya wananchi. 

“Sera ya E-Mobility inalenga kupunguza kwa kiwango kikubwa uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na matumizi ya mafuta ya petroli, huku ikisaidia sekta ya uchukuzi kuendana na teknolojia ya kisasa na kuvutia wawekezaji katika nishati safi,” amesema Chirchir.

Waziri huyo aliongeza kuwa serikali inaweka mikakati ya kuongeza vituo vya kuchaji magari na pikipiki za umeme katika maeneo mbalimbali nchini ili kurahisisha matumizi ya teknolojia hiyo. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu rafiki kwa watumiaji wa magari ya umeme, hususan katika miji mikubwa na maeneo yenye shughuli nyingi za kiuchumi.

Aidha, serikali imepanga kupunguza ushuru na tozo mbalimbali kwa magari na pikipiki zinazotumia umeme kama njia ya kuwahamasisha wananchi na wawekezaji kukumbatia teknolojia hiyo. Kupunguzwa kwa ushuru huo kunatarajiwa kupunguza gharama za umiliki wa vyombo vya usafiri vya umeme na hivyo kuongeza matumizi yake nchini.

Sera ya E-Mobility inatarajiwa pia kuchangia uundaji wa ajira mpya, kukuza ubunifu wa teknolojia na kuimarisha sekta ya nishati mbadala, huku Kenya ikiendelea kujipanga kama taifa kinara katika matumizi ya teknolojia safi barani Afrika.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!