Mgomo wa Magari ya Umma
By Dayo Radio
Published on 03/02/2026 12:42
News

Baadhi ya kaunti mbali mbali hapa nchini ikiwemo kaunti ya Nairobi zimeshuhudia mgomo wa magari ya umma mapema hii leo, hii ni baada ya wahudumu wa sekta hiyo kulalamikia dhulma wanazopitia mikononi mwa wahudumu wa bodaboda.

Kwa mujibu wa Albert Karakacha mkuu wa Matatu owners association MOA, wahudumu wa bodaboda wamekuwa wakichukua sheria mikononi kwa kuchoma magari yanayosababisha ajali na kutaka serikali kuingilia kati swala hilo ili kuhakikisha wamiliki wa magari waliopoteza magari yao wanalipwa fidia na wahusika kuchukuliwa hatua ipasavyo.

Aidha Karakacha ameeleza kuwa mgomo huo waliouanza leo utaendelea kila jumatatu ya wiki iwapo serikali haitaingilia kati swala hilo mapema iwezekanavyo.

 

" Leo tumefanya mgomo, ambao utaendelea kufanyika kila Jumatatu endapo serikali haitasikiliza malalamishi yetu. Wote walio katika sekta ya bodaboda wanaochoma magari yetu lazima wakamatwe, na magari yote yaliyochomwa lazima yalipwe fidia na serikali.”

 

Kwa upande wake mwenyekiti wa kampuni ya Forward Travellers Paul Thiongo ametoa wito wa kuachiliwa kwa magari yote yaliyokamatwa baada ya kupatikana yameegeshwa kando ya barabara katikati mwa jiji kuu la Nairobi mapema hii leo.

 

"Kuna magari mengi kutoka vyama mbalimbali vya SACCO ambayo yamezuiliwa, na yalikuwa yameegeshwa barabarani wakati wa wahudumu wa magari waligoma, tunadai yaachiliwe"

 

Ikimbukwe kuwa mgomo huo ulikuwa umeratibiwa kufanyika tarehe 28 mwezi uliopita.

Comments
Comment sent successfully!