SEKTA BINAFSI YATOA MWELEKEO WA UCHUMI WA 2026, KEPSA YASISITIZA USHIRIKIANO NA SERIKALI.
By Dayo Radio
Published on 02/02/2026 15:46
News

Muungano wa sekta binafsi nchini (KEPSA) umetaja sekta binafsi kuwa nguzo kuu ya kuchochea ukuaji wa uchumi wa Kenya mwaka 2026 na kuendelea huku ukisisitiza umuhimu wa ushirikiano thabiti kati ya serikali na wafanyabiashara.

Akizungumza wakati wa kongamano la mtazamo wa uchumi wa mwaka wa 2026 mapema leo jijini Nairobi, naib wenyekiti wa KEPSA, Bi. Brenda Mbathi, amesema kuwa licha ya changamoto za kiuchumi zinazokumba ulimwengu, Kenya ina fursa kubwa ya kuimarisha ukuaji jumuishi kupitia ubunifu na uwekezaji wa sekta binafsi.

“Biashara zinafanya kazi katika mazingira yenye changamoto nyingi zikiwemo misukosuko ya biashara ya kimataifa, masharti magumu ya kifedha na mabadiliko ya kiteknolojia, lakini ndani ya changamoto hizi kuna fursa kubwa,” amesema Bi. Mbathi.

Bi. Mbathi aidha ameeleza kuwa KEPSA ni mwavuli wa sekta binafsi nchini unaojumuisha mashirika ya wafanyabiashara wa ndani na wa kimataifa, vyama vya kitaaluma, vyumba vya biashara, kampuni kubwa, za kati, ndogo na za kuanzishwa, hatua inayoiwezesha sekta binafsi kuzungumza kwa sauti moja katika masuala ya sera na maendeleo ya uchumi.

Hata hivyo ameongeza kuwa mbali na utetezi wa sera, KEPSA hutekeleza programu mbalimbali zinazolenga kukuza uchumi na ustawi wa jamii, zikiwemo mafunzo kwa wafanyabiashara, ujenzi wa mitandao ya biashara, uhusiano wa kifedha, ushauri elekezi, pamoja na kuwaunganisha wawekezaji na masoko ya ndani na ya kimataifa.

“Tunafanya kazi kwa karibu na watunga sera ili kuboresha mazingira ya biashara, kuhimiza uwekezaji na kuiweka Kenya kama kitovu cha mikakakati za kibiashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki,” ameongeza.

Aidha amesema masuala ya kibiashara ya kikanda na bara la Afrika ni soko la Afrika Mashariki lenye zaidi ya watu milioni 300 linaendelea kutoa fursa adhimu kwa wafanyabiashara wa Kenya, huku mikataba ya kibiashara ya kikanda na bara kama vile EAC, COMESA na Mkataba wa Biashara Huria wa Afrika (AfCFTA) ikiimarisha zaidi upanuzi wa biashara.

“Ujumuishaji wa kikanda na bara unafungua soko moja kubwa la Afrika, na sekta binafsi inapaswa kuchangamkia fursa hizi ili kuongeza uzalishaji, biashara na ajira,” amesema.

Kikao hicho kimewakutanisha viongozi wa sekta ya biashara, wawakilishi wa serikali, masoko ya mitaji pamoja na washirika wa maendeleo, ambapo mijadala imelenga mtazamo wa uchumi wa kimataifa na kikanda, mchango wa masoko ya mitaji katika kukuza uchumi, pamoja na hali ya imani, ushindani na uthabiti wa sekta binafsi.

KEPSA imewahimiza wadau kuendelea kushirikiana kwa karibu, kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuunda sera rafiki kwa biashara, hatua ambayo itachangia kujenga uchumi imara, shindani na unaojumuisha mahitaji ya kizazi cha sasa na kijacho.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!