Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) imetangaza kuanza rasmi kwa mchakato wa kuwatafuta wagombea wa nafasi ya Jaji wa Mahakama ya Juu, kufuatia pengo lililoachwa na kifo cha Jaji Mohammed Ibrahim.
Kupitia notisi iliyochapishwa hii leo katika Gazeti la Serikali, Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa tume hiyo Martha Koome, amewaalika wanasheria wenye sifa na uzoefu unaohitajika kuwasilisha maombi yao ndani ya muda uliobainishwa.
Kwa mujibu wa notisi hiyo, wagombea wanapaswa kuwa na shahada ya sheria kutoka chuo kikuu kinachotambulika au wawe mawakili wa Mahakama Kuu ya Kenya. Aidha, wanatakiwa kuwa na uzoefu wa angalau miaka kumi na tano, ama kama majaji wa mahakama y a juu, wanasheria mashuhuri, wasomi wa sheria au maafisa wa mahakama.
Tume hiyo imesisitiza kuwa maombi yote yawasilishwe kabla ya tarehe ya mwisho iliyotangazwa, huku ikihimiza wanasheria wenye sifa stahiki kujitokeza ili kuimarisha utoaji wa haki nchini.
Jaji Mohammed Ibrahim, alifariki dunia Desemba 17, mwaka jana akiwa na umri wa miaka 69 alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi baada ya kuugua kwa muda mrefu.