Na Elijah Muthini
Kama wiki jana kulivyo tarajiwa kuwa na upepo mkali, wiki hii (12-19 Januari) mvua hazitarajiwi kunyesha kwa wingi, ingawa baadhi ya maeneo yanaweza kupata mvua nyepesi za asubuhi, hasa katika maeneo ya pwani na sehemu chache na vitongoji vyake. Hali hii itafanya baadhi ya siku kuwa zenye ukavu na jua ya wastani, hali inayofaa kwa shughuli za kila siku kama vile biashara za nje.
Kiwango cha juu cha joto wakati wa mchana kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 31-32°C huku joto la chini wakati wa usiku likitarajiwa kufikia hadi nyuzi joto 25°C. Hali hii ya joto ikiaashiria umuhimu wa wakaazi kuchukua tahadhari za kiafya, ikiwemo kunywa maji ya kutosha na kuepuka kukaa muda mrefu kwenye jua kali. Upepo wa wastani unatarajiwa kuvuma katika kipindi chote cha wiki kwa kasi ya 7-10(m/s) mita kwa kila sekunde.
Upepo huu unaweza kusababisha hali ya hewa kuwa na baridi kidogo nyakati za asubuhi na jioni, lakini pia unaweza kuathiri shughuli za usafiri, hususan mwanzoni mwa wiki. Katika ufuo wa bahari, mawimbi yanatarajiwa kuwa ya wastani, yakifikia kati ya futi 3.3 hadi 5.5. Hali hii ikiwa ni tahadhari kwa wavuvi, mabaharia na watumiaji wengine wa bahari, hasa wale wanaofanya shughuli kwenye maji ya kina kirefu.
Kwa ujumla, wakaazi wa Mombasa wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa, kuchukua tahadhari zinazofaa dhidi ya joto na upepo mkali, pamoja na kuhakikisha usalama wao wanapokuwa safarini katika bahari.