Taasisi ya Masoroveya humu nchini (ISK), ikiongozwa na rais wake Eric Nyadimo, kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za kitaaluma katika sekta ya ujenzi, zimelaani vikali tukio la kusikitisha la kuanguka kwa jengo lililokuwa likijengwa katika eneo la South C, jijini Nairobi.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, taasisi hizo zimeeleza masikitiko yao makubwa kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, waliojeruhiwa pamoja na jamii zilizoathirika, zikisisitiza kuwa maafa kama haya hayapaswi kuendelea kutokea katika taifa lenye wataalamu waliobobea kama Kenya.
“Tunatoa rambirambi zetu za dhati kwa familia zote zilizoathirika, na tunasisitiza kuwa kupoteza maisha kwa njia hii ni jambo lisilokubalika kabisa,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Rais wa ISK, Eric Nyadimo, amesema kuwa kuendelea kushuhudia kuporomoka kwa majengo ni ishara tosha ya kushindwa kwa mifumo ya usimamizi, maadili na utekelezaji wa sheria katika sekta ya ujenzi.

“Kuanguka kwa majengo kunadhihirisha wazi kushindwa kwa mifumo yetu ya udhibiti. Maisha ya wananchi hayawezi kuendelea kupuuzwa kwa misingi ya uzembe, tamaa na kukiuka sheria,” amesema Nyadimo.
Taasisi hizo zimewataka wataalamu wote wanaohusika katika upangaji, usanifu, ujenzi na usimamizi wa majengo kubeba jukumu lao kikamilifu, huku zikisisitiza kuwa yeyote atakayepatikana na hatia ya uzembe, udanganyifu au ukiukaji wa maadili achukuliwe hatua kali za kisheria.
“Kila mtaalamu lazima awajibike kikamilifu kwa majukumu yake. Hatutaendelea kuvumilia vitendo vya uzembe vinavyogharimu maisha ya watu,” imeongeza taarifa hiyo.
Katika taarifa hiyo, viongozi hao wameelekeza lawama kwa mifumo ya kaunti, wakisema idara za upangaji na udhibiti wa majengo hazipaswi kuonekana kama vyanzo vya mapato pekee bali kama nguzo muhimu za kulinda usalama wa wananchi.
“Idara za kaunti zinapaswa kuweka mbele usalama wa wananchi, si kukusanya mapato pekee. Ukaguzi wa majengo ni suala la maisha na kifo,” wameeleza.
Aidha, taasisi hizo zimekemea tabia ya baadhi ya waendelezaji wa miradi kukwepa uwajibikaji, zikisisitiza kuwa waendelezaji wanapaswa kubeba dhamana kamili ya kufuata Sheria ya Kitaifa ya Majengo ya mwaka 2024, ikiwemo kutoa fidia kwa waathiriwa pale ajali zinapotokea.
“Waendelezaji wa miradi lazima wawajibike kikamilifu kwa miradi yao, ikiwemo kuwafidia waathiriwa pale uzembe unapothibitika,” imesisitiza ISK.
Hata hivyo, Nyadimo pamoja na viongozi wengine wameitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo pamoja na matukio mengine ya awali, wakilalamikia kuwa licha ya zaidi ya majengo 200 kuanguka tangu mwaka 1996, mafunzo yaliyopatikana hayajatekelezwa ipasavyo.
“Tumeshuhudia zaidi ya majengo 200 yakianguka kwa miongo kadhaa, lakini mafunzo yaliyopatikana bado hayajafanyiwa kazi ipasavyo,” amesema Nyadimo.
Taasisi hizo pia zimependekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kitaifa wa upangaji na uidhinishaji wa majengo, utakaoziwezesha kaunti na serikali kuu kushirikiana, kubadilishana taarifa na kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika miradi yote ya ujenzi nchini.
Kwa pamoja, taasisi za kitaaluma katika sekta ya ujenzi zimeahidi kushirikiana na serikali ya kitaifa na zile za kaunti ili kurejesha uadilifu, usalama na imani ya wananchi katika majengo na miundombinu inayojengwa.
NA HARRISON KAZUNGU.