Gavana wa Kaunti ya Kilifi, Gideon Maitha Mung’aro, ameongoza viongozi kutoka maeneo mbalimbali ya pwani pamoja na mamia ya wananchi katika hafla maalum ya kumuenzi na kumsherehekea aliyekuwa kinara wa chama cha ODM na mwanasiasa mkongwe nchini, Baba Raila Amollo Odinga, katika maadhimisho ya kutimiza miaka 81 tangu kuzaliwa kwake.
Hafla hiyo iliyowaleta pamoja wabunge, maseneta, wawakilishiwadi, wazee wa kijamii, viongozi wa vijana na wanawake, imeelezwa kuwa si tu sherehe ya kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa, bali pia ni tukio la kuenzi safari ndefu ya uongozi, mapambano ya kidemokrasia, na mchango usiotikisika wa Raila Odinga katika historia ya taifa la Kenya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Gavana Mung’aro amesema kuwa jamii ya pwani inayo nafasi ya kipekee ya kushukuru na kumheshimu Raila Odinga kwa sababu ya nafasi alizowapatia viongozi wengi wa eneo hilo, fursa alizowafungulia na misingi ya utawala aliowajengea.

“Leo tumekusanyika hapa kama viongozi wa pwani na wanajamii kwa ujumla kumuenzi mentor wetu, jitu kubwa la siasa za Kenya, na ikoni asiye na mfano wake, Baba Raila Amollo Odinga. Baba amegusa maisha na safari za uongozi za wengi wetu, akitushika mkono, akitufungua macho, na kutembea nasi kama mzazi anayemlea mwana wake hadi akue,” amesema Gavana Mung’aro.
Ameeleza kuwa ni kupitia ushauri wa Raila Odinga ndipo viongozi wengi wa pwani waliweza kupata ujasiri wa kuingia katika siasa, kuhudumia wananchi kwa uadilifu na kupigania haki, maendeleo na usawa.

“Baba ametupatia somo muhimu kuhusu unyenyekevu, uthabiti na kupigania maslahi ya umma bila kuchoka. Ametufundisha kusimama imara hata pale ambapo njia imekuwa ngumu na hata wakati ambapo sauti zetu hazijasikika,” ameongeza.
Gavana Mung’aro amesema kuwa maadhimisho ya miaka 81 ya Raila ni wakati wa kutafakari safari ndefu aliyopitia kutoka kupigania demokrasia, kuongoza harakati za mageuzi, kufungwa jela, kupigania haki za wananchi, hadi kuwa sauti ya wanyonge bila kuchoka kwa zaidi ya miongo minne.
“Tunapoadhimisha miaka yake 81, tunatafakari juu ya urithi mkubwa alioacha urithi wa umoja, uthabiti, ujasiri na dhamira ya dhati ya kuona Kenya yenye usawa na ustawi kwa wote. Kama familia ya ODM, urithi huu unatupasa kuudumisha na kuusukuma mbele kwa nguvu mpya,” amesema Mung’aro.

Ameongeza kuwa viongozi wa Pwani wataendelea kuunga mkono maono ya Raila Odinga, wakijenga chama imara, jamii iliyoungana na utawala unaojikita katika maendeleo, uwajibikaji na kutanguliza maslahi ya wananchi.
Kwa kumalizia, Gavana Mung’aro amesema kuwa Raila Odinga atabaki kuwa kiongozi wa kizazi hiki na kijacho, mfano wa uongozi wa kujitolea, na dira ya matumaini kwa vijana na vizazi vijavyo.
“Tunamheshimu Baba leo si kwa sababu ya miaka aliyotimiza, bali kwa sababu ya maisha aliyoyatumia kwa kujitoa kwa ajili ya Kenya. Urithi wake utaendelea kutuongoza na kututia hamasa kwa vizazi vingi vijavyo,” amesema Gavana Mung’aro.
NA HARRISON KAZUNGU.