KILIFI YAZINDUA SHEHENA YA PILI YA DAWA YENYE THAMANI YA KSH 57 MILIONI KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA.
By Dayo Radio
Published on 07/01/2026 10:20
News

Kaunti ya Kilifi imepiga hatua muhimu katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya baada ya kupokea na kuzindua rasmi shehena ya pili ya bidhaa za afya kutoka Mamlaka ya Ugavi wa Dawa Nchini (KEMSA).

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, naibu gavana wa kaunti ya Kilifi Flora Mbetsa Chibule amesema hatua hiyo inaashiria dhamira thabiti ya serikali ya kaunti katika kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vyote vya afya.

Bi.Chibule aidha amesema kuwa shehena hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 57 itasaidia pakubwa kuongeza upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa vya matibabu katika hospitali za kaunti.

Ameongeza kuwa chini ya uongozi wa Gavana Gideon Mung’aro, serikali ya kaunti inaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za kitaifa kama KEMSA ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na kuhakikisha usambazaji wa mara kwa mara wa bidhaa muhimu za afya.

Akizungumzia hatua zinazofuata, Chibule amesema kwamba awamu ya tatu ya usambazaji itajumuisha bidhaa kwa ajili ya vituo 134 vya afya ngazi ya msingi, vikiwemo vituo vya afya na zahanati. Hatua ambayo inalenga kuimarisha utoaji wa huduma katika ngazi ya mashinani na kuleta huduma karibu zaidi na wananchi.

“Serikali yetu imejitolea kuhakikisha hakuna mwananchi anayeteseka kwa kukosa dawa. Tunachukua hatua za kimkakati kuhakikisha kila kituo cha afya kina vifaa na dawa za kutosha wakati wote,” amesema Chibule.

Ametoa wito kwa wahudumu wa afya na washikadau wote kuendeleza nidhamu, uwazi na uwajibikaji ili kuhakikisha bidhaa hizo zinawafikia wananchi wanaozihitaji.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!