LORI LA UVUNDO KERO KWA WAKAZI - MAGONGO.
By Dayo Radio
Published on 06/01/2026 21:03
News

Wakazi na wafanyabiashara wenye ghadhabu kali katika eneo la Magongo, kaunti ya Mombasa, wametoa malalamishi yao kufuatia uvundo mkali unaotoka kwa lori lililoegezwa kando ya barabara kutoka Changamwe kuelekea mjini.Wakazi wanasema uvundo huo umeathiri vibaya shughuli zao za kila siku na kupunguza idadi ya wateja.

“Tumeteseka kwa zaidi ya mwezi mmoja. Harufu ni kali kiasi kwamba baadhi yetu tumekuwa tukifunga biashara mapema,” amesema mmoja wa wafanyabiashara wa eneo hilo.

Uchunguzi wa mamlaka ya ukusanyaji ushuru (KRA) umebainisha kuwa mmiliki wa lori hilo alikosa kulipa ushuru wa kusafirisha kuku na mayai kutoka Taifa la Oman kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

 “Tumegundua kuwa kulikuwa na ukiukaji wa taratibu za ushuru na mzigo huo haukuidhinishwa kusafirishwa,” chanzo kutoka KRA kilidokeza.

Kwa upande wake, msimamizi wa lori hilo, Michael Omondi, aliwalaumu maafisa wa KRA kwa kuondoka bila kutoa mwongozo wa hatua zinazofaa kuchukuliwa.

 “KRA walichukua stakabadhi na kuondoka bila taarifa yoyote ya makubaliano. Sasa mzigo umeharibika na mimi ndiye ninayebeba hasara,” alisema Omondi.

Aidha, Omondi ametaja kuwa ameathirika kifedha na sasa anaitaka serikali kumfidia.

“Ninahitaji fidia ya shilingi milioni moja na laki mbili. Hiyo ndiyo hasara ambayo nimepata ndani ya mwezi mmoja,” ameongeza.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!