Akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini Nairobi, Msemaji wa Serikali Dkt. Isaac Mwaura amesema kuwa hadi sasa Serikali imefanikiwa kuunda zaidi ya ajira milioni mbili katika sekta mbalimbali.
"Serikali imeunda zaidi ya ajira milioni mbili ndani na nje ya nchi, ishara kwamba tumetoka katika hatua ya kujijenga upya kiuchumi na sasa tuko kwenye awamu ya ukuaji endelevu.”
Ameeleza kuwa Kenya inaelekea kuachana na uchumi wa Dunia ya Tatu na kuelekea uchumi wa Dunia ya Kwanza unaozingatia uzalishaji, uhuru wa kiuchumi na upatikanaji wa fursa kwa wananchi wote.
“Ajenda ya BETA ndiyo injini kuu ya mageuzi haya kwa sababu inapanua upatikanaji wa mitaji, masoko, ujuzi na teknolojia kwa mamilioni ya Wakenya waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa uchumi,” amesema Dkt. Mwaura.
Amesisitiza kuwa tofauti ya msingi kati ya nchi zinazoendelea na zilizoendelea si rasilimali, bali ni ushiriki wa wananchi.
“Kupitia uthabiti wa uchumi mkuu, urasimishaji wa biashara na matumizi ya teknolojia serikalini, tunajenga uchumi wa kisasa, shirikishi na unaoongozwa na wananchi,” amefafanua.
Kwa mujibu wake, miezi kumi na miwili iliyopita imekuwa kipindi cha mageuzi makubwa katika utekelezaji wa ajenda ya BETA.
“Baada ya changamoto za ndani na nje ya nchi, sasa tumeingia kwenye awamu ya uthabiti wa uchumi tukitegemea usimamizi madhubuti na uwekezaji unaomlenga mwananchi,” amesema.
Ameongeza kuwa viashiria vya uchumi vinathibitisha hali hiyo. “Mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 9.6 hadi asilimia 4.6, jambo ambalo limeongeza nguvu ya ununuzi kwa familia nyingi. Shilingi nayo imeendelea kuwa thabiti kutokana na mauzo ya nje na rekodi ya fedha kutoka kwa wakenya wanaoishi ughaibuni,” amesema, akibainisha kuwa fedha hizo zimefikia shilingi bilioni 638 katika mwaka wa fedha uliopita.
Kuhusu mwasuala ya miundombinu, Dkt. Mwaura amesema Baraza la mawaziri limeidhinisha kuanzishwa kwa Mfuko wa jitaifa wa miundombinu.
“Huu ni uamuzi wa kihistoria katika safari ya Kenya kuelekea hadhi ya Dunia ya Kwanza. Mfuko huu wa trilioni tano utaoanisha rasilimali za umma na sekta binafsi ili kufadhili miradi yenye athari kubwa,” amesema.
Ameeleza kuwa Serikali inalenga kuondokana na utegemezi wa mikopo kupitia uuzaji wa kimkakati wa mali za umma zilizopevuka, kuhamasisha akiba za ndani na kupanua umiliki kupitia masoko ya mitaji.
“Rasilimali zitakazopatikana zitaelekezwa moja kwa moja katika miradi ya umwagiliaji, usafiri, usafirishaji na nishati ili kuimarisha uzalishaji,” amesema.
Amesema mpango wa BETA unaendelea kujenga msingi wa uchumi jumuishi unaonufaisha familia za wakenya.
“Tumejizatiti katika utekelezaji wenye nidhamu, uwajibikaji na ushirikiano ambao unamweka mwananchi katikati ya maendeleo ya taifa,” amesema.
Aidha, amesema Kenya inalenga kufikia hadhi ya nchi kama Singapore kama ilivyowekwa wazi na Rais William Ruto.
“Rais hana nia ya kuongeza muda wa uongozi wake. Anataka kutimiza malengo yake yote ndani ya kipindi cha kikatiba,” amesema Dkt. Mwaura
NA HARRISON KAZUNGU.