MWAKILISHI WADI WA VIJANA KAYAFUNGO IRINE AMINA KAZUNGU AANZA UKAGUZI WA MIRADI RASMI.
By Dayo Radio
Published on 12/12/2025 07:05
News

Mwakilishi wadi wa Vijana wa Kayafungo eneobungela Kaloleni, Irine Amina Kazungu, ameanza rasmi ziara ya kukagua na kufuatilia miradi ya maendeleo katika wadi hiyo, kufuatia makabidhiano ya orodha ya miradi kutoka kwa mwakilishi wa sasa, Agnes Sidi. 

Katika hatua yake ya kwanza, Amina ametembelea zahanati ya Gotani, na kuthibitisha kwamba jengo la uzazi lililojengwa katika kituo hicho ni mradi uliotekelezwa na mwakilishi wadi Agnes Sidi chini ya serikali ya Kaunti ya Kilifi.

Kulingana naye uongozi wa hospitali umeeleza kuwa ujenzi wa jengo jipya ulikuwa wa dharura kutokana na lile la awali kupata nyufa nyingi zilizohatarisha maisha ya kina mama na watoto wanaotegemea huduma za kituo hicho.

Hata hivyo katika ziara yake Amina amegundua kuwa wanaotegemea kituo hicho wanapitia changamoto kubwa zinazohitaji hatua za haraka ikiwemo tanki kuu la kuhifadhia maji katika kituo hicho akitaja lilipata nyufa na kuanguka, na kusababisha upungufu mkubwa wa maji safi.

Aidha amebaini kuwa kisima kilichopo ndani ya zahanati hiyo hakifanyi kazi, jambo ambalo limewalazimu wafanyakazi na jamii kutafuta vyanzo vingine visivyo salama na visivyotegemewa.

Wakati uo huo Amina ataja kuwa changamoto hizo zimeathiri kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma za afya, hasa katika kitengo cha uzazi ambacho kinahitaji maji safi kila wakati ili kuhakikisha usalama wa mama na mtoto.

Kutokana na hali hiyo, Irine ametoa wito kwa mwakilishi wadi Agnes Sidi na mbunge wa eneobunge la Kaloleni Paul Katana kuweka kipaumbele katika kushughulikia matatizo wanayopitia wakaazi wa Kayafungo kupitia mgao wa fedha za NG-CDF zinazotolewa kupitia ofisi ya mbunge na rasilimali za maendeleo za kaunti zinazodhibitiwa na mwakilishiwadi akisema kuwa inawezekana kurejesha tanki la maji na kukarabati kisima ili zahanati ya Gotani iweze kurejea katika utoaji wa huduma bora na salama kwa jamii.

“Wakaazi wa Kayafungo tuna haki ya kuelewa majukumu ya viongozi wetu, lakini pia tuna wajibu wa kuwaunga mkono wanapopigania rasilimali za maendeleo. Tukishirikiana, tunaleta mafanikio ya pamoja.” amesema Amina.

Amesisitiza kuwa wakaazi wa Kayafungo wana haki ya kufahamu majukumu ya viongozi wao na kuwawajibisha na kusema kwamba wana jukumu la kuwaunga mkono viongozi wao wanapopigania rasilimali kwa ajili ya maendeleo. 

Kwa kauli yake, Amina amesema kwamba maendeleo ya kweli yanapatikana pale ambapo viongozi na wananchi wanashirikiana kwa ukaribu na akahitimisha kwa kusisitiza kuwa ataendelea na ziara zake kuhakikisha kila mradi unaonufaisha jamii unafanyiwa tathmini na kuimarishwa kadri inavyohitajika.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!