Mashirika na wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu wamebaini kuwa ukosefu wa mataa ya barabarani, almaarufu mulika mwizi, umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la visa vya uhalifu katika wadi ya Mjambere eneobunge la Kisauni, Kaunti ya Mombasa.
Akizungumza na waandishi wa habari, mwanaharakati Ahmed Mbaraki amesema kuharibika kwa mataa hayo kumeongeza visa vya utovu wa usalama, jambo ambalo limezua hofu kwa wakazi hususan kipindi hiki cha msimu wa sherehe za krisimasi.
“Mata ya mitaani yameharibika na hali ya usalama imezorota. Tunaitaka serikali ya kaunti kuyarejesha ndani ya wiki moja, hasa tukizingatia msimu huu wa sikukuu ambao huambatana na shughuli nyingi za usiku,” amesema Mbaraki.
Kwa upande wake, Robin Obaga kutoka shirika la Ajenda Kenya amesisitiza umuhimu wa hatua za dharura kuchukuliwa ili kukarabati mulika mwizi hao katika maeneo yote ya Kisauni.
“Kisauni tayari inajulikana kwa changamoto za uhalifu, na ukosefu wa mwanga unazidisha hali. Tumeshapeleka malalamishi katika ofisi za wadi ya Mjambere na tumeahidiwa kwamba ndani ya wiki moja mataa haya yatarejea kufanya kazi,” amesema Obaga.
Kauli hii imeungwa mkono na Vivian Akoth, mkazi wa Kadongo, wadi ya Mjambere, ambaye ameeleza kuwa athari za ukosefu wa mwanga zimesababisha kushuka kwa biashara za usiku.
“Biashara zetu zimezorota kwa sababu vijana wa mapanga wameongezeka gizani. Bila mwanga, hatuwezi kufanya kazi hadi usiku kama ilivyokuwa hapo awali,” amesema.
Wanaharakati hao sasa wanaitaka serikali ya kaunti kuchukua hatua za haraka kurejesha usalama kwa kuimarisha miundombinu ya taa za barabarani kabla hali haijazidi kuwa mbaya.
NA HARRISON KAZUNGU.