Shirika la ajira la BrighterMonday Kenya, kwa ushirikiano na Mastercard Foundation kupitia mpango wa Gen-Kazi chini ya EmpowerHer Initiative, limezindua rasmi Mombasa Career Clinic & Entrepreneurship Summit hatua mahususi inayolenga kuongeza ushiriki wa wanawake vijana katika sekta ya utalii na ajira zenye staha katika Kaunti ya Mombasa.
Uzinduzi huu umefanyika wakati ambapo kaunti ya Mombasa inakabiliwa na kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, kinachofikia asilimia 44%, hali inayodai mbinu jumuishi na endelevu za kiuchumi ili kuwawezesha vijana wanawake kupata nafasi za ajira na ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa ya soko.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Geraldine Chepchirchir, Mtaalamu Mwandamizi wa Mipango katika BrighterMonday Kenya, amesisitiza nafasi muhimu ya wanawake katika uchumi wa utalii ukanda wa Pwani.
“Wanawake ndio uti wa mgongo wa sekta ya utalii na ukarimu katika eneo la pwani, lakini bado wanakabiliwa na vikwazo vinavyowazuia kupata ajira zenye heshima, uhaba wa ujuzi, ukosefu wa ushauri, changamoto za usalama na nafasi chache za uongozi. Kupitia EmpowerHer, tumejizatiti kubadilisha hali hii kwa kuwapa wanawake ujuzi wa ajira, maarifa ya kibiashara, stadi za kidijitali na ushauri wa kaunti ili washiriki kikamilifu katika sekta ya utalii.”

Kwa mujibu wa takwimu za KNBS (2023), wanawake wanachangia karibu nusu ya nguvu kazi nchini, lakini bado wengi wao hawapati nafasi katika ajira rasmi wala ujasiriamali wa kiwango cha juu, hususan katika sekta ya utalii ambapo ni njia moja ya sekta zinazoongoza kiuchumi eneo la pwani.
Programu ya EmpowerHer inalenga kupunguza pengo hilo kwa kutoa mafunzo, kuwajengea uwezo na kuweka mifumo ya ushauri itakayosadia kupiga hatua na kusaidia kuinua malengo yanayodhamiriwa.
Mradi huu unalenga kuwafikia wanawake 217,000 katika kaunti zote 47 ndani ya kipindi cha miezi 18, ukiwapa zana na mbinu za kuwasaidia kujiendesha katika soko la ajira linalobadilika na kutambua fursa mpya, ikiwemo zile zinazoibuka katika sekta ya utalii na uchumi samawati.
Kupitia mpango wa Gen-Kazi, BrighterMonday Kenya inaendeleza mpango mpana wa kuwawezesha vijana wenye umri wa miaka 18–35, kwa kuzingatia makundi yaliyotengwa zaidi; asilimia 70% wanawake, 70% vijana wa maeneo yasiyo ya mijini, na 10% watu wenye ulemavu, kwa lengo la kuongeza fursa za ajira zenye staha na kuimarisha biashara zinazomilikiwa na wanawake vijana.
NA HARRISON KAZUNGU.