Naibu Gavana wa Kaunti ya Kilifi ameongoza kikao maalum kilichowaleta pamoja washika dau mbalimbali wa muziki na sanaa, ambapo ametangaza rasmi hatua mpya ya kaunti katika kuwaendeleza vijana kupitia vipaji vyao.
Katika kikao hicho, ametangaza kuwa Serikali ya Kaunti ya Kilifi imesaini Mkataba wa Maelewano (MoU) na Mseto Ventures Limited (Mseto East Africa) kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Kutafuta na Kukuza Vipaji vya Muziki na Neno la Kutamkwa.

“Huu ni mwanzo wa safari mpya ya kuinua vipaji vya vijana wetu. Tunataka kila kijana mwenye kipaji apate nafasi ya kuonekana, kuimarika na kufikia ndoto zake kupitia mazingira tuliyoyaweka.”
Hata hivyo amefafanua kuwa mpango huo umeundwa mahsusi ili kutambua, kulea, na kuwawezesha vijana walio na vipaji mbalimbali kwa kuwapatia ushauri wa kitaalamu, mafunzo ya kimkakati, na nafasi za kupata mwanga mpana katika tasnia ya ubunifu.
Ameeleza kuwa programu hii ni sehemu ya mikakati ya kaunti ya kukuza sekta ya ubunifu kama njia muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Kilifi ina hazina kubwa ya vipaji. Ushirikiano huu na Mseto East Africa ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kuhakikisha vipaji hivyo havipotei bali vinageuka kuwa fursa halisi za ajira na maendeleo.”
Uzinduzi rasmi wa programu hiyo utafanyika tarehe 13 Disemba katika Uwanja wa Water, Kilifi Mjini, ambapo ametaka vijana kujitokeza kwa wingi ili kufaidika na fursa hiyo.
Hatua hii muhimu imekuja siku chache baada ya ofisi yake kuwakaribisha wajumbe wa Kilifi Rising Stars ukiongozwa na mtangazaji maarufu Mzazi Willy M. Tuva, ambapo walijadiliana mbinu za kimkakati za kuwawezesha vijana wenye vipaji na kuibua nafasi zaidi za ukuaji wao katika sanaa.

Amesisitiza kuwa serikali ya kaunti itaendelea kushirikiana na wadau wa muziki na sanaa kwa ujumla ili kuhakikisha vijana wanapata mazingira bora ya kukuza vipaji vyao na kugeuza uwezo huo kuwa fursa za kimaendeleo.
NA HARRISON KAZUNGU.