KILIMO CHA MAKUBALIANO KUPATA MWELEKEO MPYA BAADA YA KONGAMANO LA ICCF 2025 KUFANYIKA NAIROBI.
By Dayo Radio
Published on 19/11/2025 06:45
News

Kongamano la kimataifa kuhusu kilimo cha makubaliano (International Conference on Contract Farming – ICCF 2025) limefanyika leo tarehe 18 Novemba 2025 Nairobi, likiwakutanisha wadau muhimu wa sekta ya kilimo kutoka ndani na nje ya nchi.

Washiriki walijumuisha wakulima, wajasiriamali wa kilimo, watunga sera, wawekezaji, mashirika yasiyo ya kiserikali, wataalamu wa ubunifu wa teknolojia za kilimo, watafiti pamoja na washirika wa maendeleo, ambao wote walijadiliana kwa kina kuhusu mustakabali wa contract farming na umuhimu wake katika kuinua uchumi wa kilimo.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari washiriki wametoa maoni, mapendekezo na mikakati kabambe ya kuhakikisha mfumo wa kilimo cha makubaliano unaleta manufaa ya haki kwa pande zote kupitia kuweka misingi imara ya mkataba, kuongeza uelewa wa kisheria, kuimarisha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi, kukuza uwazi na uwajibikaji, na kuchochea matumizi ya teknolojia za kisasa kama digital contracting na mifumo ya uzalishaji iliyoendelezwa kiteknolojia.

Aidha, suala la kuwawezesha wakulima wadogo kupitia elimu, upatikanaji wa rasilimali, huduma za kifedha na bima ya kilimo limepewa kipaumbele ili kuhakikisha hawaachiwi nyuma katika masuala ya kukuza uchumi wa taifa.

Kwa ujumla, washiriki wamesema kuwa iwapo mapendekezo hayo yatatekelezwa ipasavyo, sekta ya kilimo nchini na kimataifa itafunguka zaidi, kuongeza tija, kuongeza ubunifu, na kuhakikisha wakulima wananufaika kiuchumi bila kupoteza haki zao za kimsingi.

Hata hivyo kongamano hilo linaendelea hadi siku ya kesho ambapo mwongozo rasmi, maazimio pamoja na mpango wa utekelezaji unatarajiwa kutangazwa.

 

HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!