KILIFI YAANZA SAFARI YA MAPINDUZI YA NISHATI SAFI KUPITIA MRADI MPYA WA UK PACT.
By Dayo Radio
Published on 19/11/2025 06:42
News

Idara ya Nishati Kaunti ya Kilifi imeanza rasmi utekelezaji wa juhudi mpya za mageuzi ya nishati safi kupitia mradi wa UK PACT 1, hatua ambayo imezinduliwa katika kikao maalum cha County Level Project Inception Meeting.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari ni kwamba uzinduzi huo umefanyika kwa ushirikiano na mashirika ya Practical Action, Gamos East Africa, Clean Cooking Association pamoja na wadau wengine muhimu kutoka sekta binafsi, mashirika ya kijamii, watafiti, vijana na wawakilishi wa serikali za mitaa.

Mradi huu unaojulikana kama Enhancing Local Manufacturing and Energy Crop Cultivation for Clean Cooking Supply Chains (ELMECC) umebuniwa kwa lengo la kuimarisha uzalishaji wa ndani wa vifaa na teknolojia za nishati safi sambamba na kukuza kilimo cha mazao yanayotumika kuzalisha nishati mbadala. Kupitia mradi huu, Kaunti ya Kilifi inalenga kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati vinavyochochea uharibifu wa misitu kama vile kuni na mkaa, na badala yake kuweka msingi wa upatikanaji wa nishati safi, salama, nafuu na rafiki kwa mazingira.

Utekelezaji wa mradi wa ELMECC ni sehemu ya hatua za kimkakati za kufanikisha Kilifi County Energy Plan, mpango ambao unaweka mwelekeo wa mabadiliko makubwa katika sekta ya nishati kwa kuzingatia kuirikisha jamii, utafiti unaotegemea ushahidi, maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati (SMEs), na uanzishaji wa fursa mpya za ajira na biashara. Kupitia juhudi hizi, kaunti inatarajia kufungua njia ya ukuaji wa kiuchumi, kuimarisha usalama wa chakula, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuboresha afya ya jamii kwa kupunguza athari zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo salama majumbani.

Wadau waliohudhuria wameelezea matumaini makubwa kuwa mradi huu utafungua upeo mpya wa ubunifu, utaongeza thamani ya uzalishaji wa ndani, na kuchochea ushirikiano mpana kati ya sekta binafsi na serikali, huku ukiwajengea uwezo washiriki wa teknolojia ya nishati safi na kilimo cha mazao ya nishati kama njia endelevu ya kujitegemea kiuchumi.

Hata hivyo wamesema kuwa huu ni mwanzo wa safari ya mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kimazingira katika kaunti ya Kilifi, safari inayojengwa juu ya ushirikiano, malengo ya muda mrefu na maono ya kuhakikisha jamii zinafikia nishati safi kwa matumizi ya nyumbani na kibiashara.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!