SERIKALI YAHAIDI MAGEUZI MAKUBWA KUPITIA UCHIMBAJI WA DHAHABU KAKAMEGA.
By Dayo Radio
Published on 17/11/2025 19:12
News

Msemaji wa Serikali, Dkt. Isaac Mwaura, amesema kuwa Serikali inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya eneo la Ikolomani, Kaunti ya Kakamega, huku miradi 77 ikiwa inaendelea kutekelezwa kwa wakati mmoja. Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa kiwanda cha uchimbaji na usafishaji wa dhahabu ambacho kiko katika hatua ya asilimia 88 kukamilika kwa gharama ya shilingi milioni 129.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari baada ya kuzuru katika kaunti ya Kakamega wakati wa ziara yake, Dkt. Mwaura amesema kuwa ugunduzi wa dhahabu yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 683 ni hatua kubwa ya mageuzi ambayo itawaletea manufaa wakazi wa eneo hilo pamoja na taifa zima.

Ameeleza kuwa mgao wa wa madini hayo utafanyika kwa mujibu wa Sheria ya madini sura ya 306 ambapo serikali kuu, kwaushirikiano na serikali ya kaunti na jamii za wachimbaji wote watanufaika kwa uwiano uliowekwa kisheria.

Ha hivyo amefafanua pia kuwa wawekezaji wote watatakiwa kutenga asilimia moja ya mauzo yao ya jumla kwa ajili ya mkataba wa maendeleo ya jamii ambao utasimamiwa na kamati yenye wanachama 14, ili kuhakikisha kwamba jamii inashirikishwa na inanufaika moja kwa moja na rasilimali hizo. Dkt. Mwaura amesema kuwa hazina ya taifa tayari imefungua akaunti maalum kwa ajili ya kukusanya mapato ya hayo huku mfumo wa kugawanya fedha hizo ukiwa katika hatua za mwisho kukamilishwa.

Vile vile ameongeza kuwa serikali inaandaa mpango rasmi wa ununuzi wa dhahabu kupitia kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Kakamega kwa ushirikiano na benki kuu ya Kenya, hatua ambayo inalenga kutoa thamani halisi kwa wachimbaji na kuzuia hasara zitokanazo na ulanguzi ama bei za kudhulumu. 

Zaidi ya kiwanda hicho, Serikali inaendelea kutekeleza miradi mingine ya maendeleo ambapo inajenga masoko, hosteli, barabara, miradi ya maji, hifadhi za kuendeleza na kuchakata mazao pamoja na maeneo maalum ya uzalishaji kwa ajili ya uagizaji nje kama ule wa Nasewa katika Kaunti ya Busia.

Dkt. Mwaura aidhq amepongeza kasi ya maendeleo yanayoendelea kushuhudiwa katika eneo la Magharibi na kusisitiza kuwa serikali imejikita katika kuhakikisha usawa wa mgao wa rasilimali na maendeleo katika kila kaunti nchini. Aidha, ametoa hakikisho kwamba serikali italipa fidia kwa wamiliki wa ardhi wote watakaoathiriwa na utekelezaji wa miradi hiyo.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!